Azam FC, KMKM wakamiana

Muktasari:

Kocha wa Azam, Hans Pluijm alisema amefurahishwa kutinga hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa mabao 2-1.

MABINGWA wateteti wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC na timu ya Jeshi ya KMKM wataanza kucheza nusu fainali za michuano hiyo leo Ijumaa mchana na kila timu imetamba kushinda ingawa KMKM imepania zaidi.

KMKM ilitinga hatua hiyo ikishika nafasi ya pili Kundi A ikiwa na pointi nne wakati Azam iliongoza Kundi B ikivuna pointi saba sawa na Malindi ingawa tofauti yao ilikuwa ni mabao ya kufunga na kufungwa.

Kocha wa Azam, Hans Pluijm alisema amefurahishwa kutinga hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa mabao 2-1.

“Tumeingia hatua ya nusu fainali, ni hatua ngumu ingawa michuano ina changamoto kubwa hasa upinzani kutokana kwenye timu tulizokutana nazo, lakini tumejipanga kupata ushindi kwenye mechi hiyo ili tuingie hatua ya fainali na kutetea ubingwa wetu.

“Kiwango cha wachezaji sijaridhishwa nacho sana kwasababu baadhi ya mechi wanacheza vizuri na nyingine wanacheza chini ya kiwango. Hilo ni tatizo kuelekea mechi za huko mbele ambazo ushindani utakuwa mkali zaidi.

“Wapinzani wetu tunaokwenda kukutana nao ni wazuri na tumewaona walivyocheza mechi zao za awali kwenye kundi lao, sio timu ya kuibeza, hivyo tunapaswa kuwa na maandalizi mazuri,” alisema Pluijm.

Kwa upande wa Kocha wa KMKM, Ame Msimu alisema; “Tangu mwanzo tumewaona Azam jinsi wanavyocheza, tunafahamu mbinu zao na mchezaji mmoja mmoja tumewangalia.

“Tumegundua nguvu zao nyingi wanaziweka kwa wachezaji wachache kama Obrey Chirwa na Donald Ngoma katika ufungaji lakini bado wana mapungufu kiasi ambayo tumeyagundua,” alisema Msimu

Msimu alisema kutokana na uzito wa mechi hiyo atatumia kikosi chake kilichocheza mechi dhidi ya Simba kilichofungwa bao 1-0 kwa kuwa ana vikosi viwili.