Azam, Man City pacha, lakini mmoja mkaidi

Muktasari:

  • Kiuhalisia wakati Azam anapambana kuzitoa Simba na Yanga kwenye kiti chao cha enzi, Manchester City ilikuwa inatakiwa kupambana na Top Four ya Manchester United, Chelsea, Arsenal na Liverpool.

Dar es Salaam.Msimu wa 2008-2009, soka la Tanzania ilisemekana linapata mwanga mpya hususani kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Kulikuwa na klabu ambazo zilionekana kujakuwa Manchester City ya ligi yetu na Paris ST Germain kwa wakati mmoja.

Naam mzee wetu Said Bhakresa alikuwa amewekeza kwenye klabu ya Azam, na pia upande wa pili tajiri aliyeaminika kuwa mpenda soka, Mo Dewji alikuwa amewekeza kwenye klabu ya African Lyon.

Ni klabu ambazo iliaminika kuwa pengine zilikuwa zinakuja kuleta mfumo mpya na mwonekano mpya wa ligi yetu ikiwa pia ni pamoja na kuongeza ushindani wa kiuwekezaji na biashara kwa ujumla na hata udhamini kwa klabu zingine ingawa mmoja aliamua kujichagulia kifo mapema.

Kule kwenye Ligi Kuu England, wakati Azam inapanda daraja chini ya uwekezaji wa mzee Bakhresa, Manchester City iliyokuwa goigoi ilikuwa inanunuliwa na tajiri Sheikh Mansour.

Kiuhalisia wakati Azam anapambana kuzitoa Simba na Yanga kwenye kiti chao cha enzi, Manchester City ilikuwa inatakiwa kupambana na Top Four ya Manchester United, Chelsea, Arsenal na Liverpool.

Mpango wa kwanza wa Sheikh Mansour ilikuwa kuleta wataalamu wa soka kutoka kwenye klabu zilizokuwa vimefanikiwa kama Barcelona na kuhakikisha kuwa wana mpango kazi wa kipindi kirefu.

Hawa ndio ambao walikuwa wanaamua Manchester City inakwenda wapi na kwa muono upi ambao ungekuwa tofauti na vilabu vingine vilivyokuwepo.

Hao wakatwaa ubingwa wa ligi kuu ya nchini England baada ya misimu minne tangu kununuliwa na Sheikh Mansour.

Azam kwa upande wao, walitwaa ubingwa msimu wa mwaka 2014 ikiwa ni misimu sita tangu waingie kwenye Ligi Kuu Bara ambayo sio mbaya kwa sababu walikuwa na kile unachoweza kukiita “ugeni wa ligi” hivyo walikuwa ni kuku wageni na kamba mguuni mwanzoni ingekuwa halali yao.

Tangu hapo hali imekuwa tofauti kwani hawakutwaa ubingwa wa ligi tena wakati Manchester City ikiendelea kuwepo kwenye ligi ya mabingwa na kutwaa ubingwa mara mbili zingine na mara ya mwisho ikiwa ni kwa rekodi ya pointi ambayo haikuwahi kuwekwa hapo kabla achilia mbali zaidi ya magoli mia moja ambayo pia ni rekodi.

Kwa sasa huwezi kutaja klabu bora England pasipo kuanza na Manchester City lakini unaweza kuwa salama kabisa kutaja Simba na Yanga kwa mpangilio wowote unaohitaji kisha ukataja Azam bila ya madhara yoyote. Tafsiri yake ni nini? Picha kubwa inaendelea kuwepo kuwa Tanzania hatuna weledi kwenye kuongoza taasisi za michezo na kuzisimamia.

Kama wenye elimu ya usimamizi wa michezo wapo basi hawatufai kwani wameshindwa kutumia taaluma yao kuwa wenye manufaa.

Kingine ni kuweka “ushikaji” kwenye usimamizi wa klabu hivi na ndio maana neno “figisu” limekuwa neno linalopendwa kwenye masuala ya kiuongozi Tanzania.

Nimehesabu vidole vya kiganja changu na kukamilisha hesabu ya kwanza ya mtoto kujifunza yaani namba kumi kumaanisha umri ambao Azam imekuwepo kwenye ligi na kushindwa kugawana ubabe na klabu hizi mbili.

Pale England tangu Sheikh Mansour aingie, Manchester City imetwaa ubingwa mara tatu sawa na Chelsea na Manchester United, na tangu watawae ubingwa ni Chelsea pekee ambayo imetwaa mara mbili, huku wao wakitwaa mara mbili pia. Hii inaonyesha nguvu na majibu ya mipango mizuri ya uwekezaji na kuwa na wasimamizi wazuri wenye maono ya mbali kwenye uwekezaji.

Michezo imekuwa sayansi siku hizi ambayo ukiifuata kienyeji inakuchapa fimbo na unabaki usifahamu lipi sahihi la kufanya. Azam ilitakiwa iwe imerejesha akili muda mrefu kwenye vichwa vya vilabu vingi Tanzania, ilitakiwa iwe mfano wa kuigwa kwenye kufanya vyema kwenye ligi ya mabingwabarani Afrika.

Leo hii tunaogopa mafanikio ya TP Mazembe, Mamelodi Sundowns, hata AS Vita inazungumzwa kwa mafanikio lakini hakuna cha ajabu zaidi ya umakini na watu wa mpira kufanya kazi yao inavyopasa kuwa.

Azam na Manchester City ni mapacha kabisa kwa maana ya uwekezaji, tatizo mmoja ameamua kuwa mkaidi, ameshindwa kufuata misingi ya usimamizi kwenye soka.