Ayaa Yanga washtukiwa buana!

Muktasari:

  • Mwanaspoti linafahamu, Yanga ilikuwa ikimpigia hesabu winga machachari wa KMC, Hassan Kabunda ili kuwa naye katika msimu ujao, lakini viongozi wa timu hiyo ya Manispaa wakagomea kiaina.

YANGA imepania nyie acheni tu. Unajua hesabu za sasa za mabosi wapya wa klabu hiyo ni kuhakikisha msimu ujao wanakuwa na kikosi kimoja matata sana, fasta wakaanza mipango ya kusaka nyota wapya na jicho lao lipo kwa klabu za Ligi Kuu Bara.

Unaambiwa kwa sasa hesabu ni kutaka kuchomoa baadhi ya wachezaji wa KMC, lakini wakakutana na kigingi bab’kubwa baada ya mabosi wa Kinondoni kushtukia mchezo na fasta kuitana ili kuweka mambo sawa ili nyota wao wasichomolewe.

Mwanaspoti linafahamu, Yanga ilikuwa ikimpigia hesabu winga machachari wa KMC, Hassan Kabunda ili kuwa naye katika msimu ujao, lakini viongozi wa timu hiyo ya Manispaa wakagomea kiaina.

Licha ya Yanga kuwa tayari kuvunja benki ili kumng’oa mtoto huyo wa nyota wao wa zamani, Salum Kabunda ‘Ninja’, lakini Jangwani wamekutana na kigingi cha mabosi wa KMC kuwaita nyota wao wote ili kuzungumza nao kuwapa mikataba mipya.

Asilimia kubwa ya wachezaji wa KMC wamesainishwa mikataba ya mwaka mmoja ambayo inaishia mwishoni mwa msimu huu, lakini katibu mkuu wa timu hiyo, Walter Harrison alifichua tayari wameshakaa chini kama viongozi ili kuwakabiza nyota wao.

“Tayari tumeshakaa chini kama viongozi na kufanya vikao vya ndani kwa ndani kwaajili ya kufanya maandalizi ya mapema ya msimu ujao, nakuhakikishia wachezaji ambao tunataka kuendelea nao msimu ujao hawatoondoka,” alisema.

Aliongeza hawawezi kuzuia watu kuzungumza kama mchezaji lakini wao wanachofanya ni kuhakikisha mchezaji wanayemtaka wanaendelea naye.

Akizungumzia kuhusu kuhusu msimu ujao, alisema; “Tunataka kuendeleza makali yetu kwa msimu ujao na kuwa na timu bora zaidi ya msimu huu ili kuzidi kuleta ushindani katika ligi.”