Aussems awazuga Azam FC

Friday August 16 2019

 

By Olipa Assa

UKISIKIA kuchezwa shere ndiko huku, baada ya Kocha wa Simba, Patrick Aussems kuwazuga Azam akidai anawahofia kuelekea mchezo wao wa Ngao ya Jamii utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa.
Aussems amesema uwepo wa kocha mpya ndani ya Azam, Etienne Ndayiragije anaamini wapinzani wao watakuja na mbinu mpya ambazo zinaweza kuwasumbua tofauti na walivyokutana nao kwenye msimu uliopita. Hata hivyo rekodi za Ndayiragije dhidi ya Simba zinaonyesha hajawahi kuibuka na ushindi hata mchezo mmoja tangu alipokuwa Mbao kabla ya kuinoa KMC msimu uliopita.
Kocha Aussems amesema wanacheza na Azam, mechi ya ngao jamii hivyo anaamini itakuwa na mabadiliko kwa madai kila kocha anakuwa na mbinu zake.
Mbali na mabadiliko anayoamini kocha Ndayiragihe atakuwa nayo, pia amesema Azam FC imetoka kucheza Kombe la Kageme, analoamini litakuwa limewajenga kimbinu.
"Itakuwa mechi ngumu ila kwetu ni jambo zuri kwa sababu itatusaidia kutuweka sawa kwa ajili ya mechi yetu marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo.
"Kucheza na Azam FC ni kipimo kizuri kwetu kujua tunahitaji kubadilisha nini juu ya mechi ya kimataifa, kikubwa tunaamini tutapata nafasi ya kusonga mbele," amesema.

Advertisement