Aussems awatibua vigogo huko Simba, kupewa barua leo

Muktasari:

Uongozi wa Simba ulimsimamisha kazi kocha huyo raia wa Ubelgiji baada ya mechi yao na Ruvu Shooting licha ya ushindi wa mabao 3-0.

SIKU moja baada ya kuwekwa kitimoto, kocha wa Simba, Patrick Aussems ameandika kwenye mitandao yake ya kijamii kuwaeleza mashabiki wa timu kwamba, angependa kuendelea kuifundisha timu lakini bodi imemsimamisha kazi.

Aussems ameeleza kwamba anaamini kama angeendelea kuifundisha timu hiyo, basi wangeona soka la kuvutia na kutwaa makombe mbalimbali ambayo timu yao ingeshiriki.

Juzi Alhamis, Aussems alikutana na Bodi ya Wakurugenzi ya Simba akiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingiza ambao walimtaka ajieleze ni kwanini aliondoka katika kituo cha kazi bila kufuata utaratibu na jana walikutana tena kupitia na kuchambua kwa kina utetezi wake ili leo Jumamosi watoe uamuzi. Aussems aliondoka nchini ambapo ilidaiwa alikwenda Afrika Kusini kufanya mazungumzo na moja ya klabu za huko huku akimuaga mwajiri wake kwa njia ya barua pepe akiwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere na kwamba, amepata dharura na angerejea baada ya siku tatu.

Alipoulizwa juu ya andiko lake, Aussems alisema: “Nimeandika tu, lakini tusubiri kitakachoamuriwa na viongozi, hivyo tujipe muda.”

Uongozi wa Simba ulimsimamisha kazi kocha huyo raia wa Ubelgiji baada ya mechi yao na Ruvu Shooting licha ya ushindi wa mabao 3-0.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kwamba Aussems ni kama anatafuta huruma ya mashabiki wake ili aonekane hana makosa ingawa kwenye kikao hicho alishindwa kujibu maswali aliyokuwa akihojiwa.

Kwa mujibu wa kiongozi mmoja wa juu, inadaiwa kwamba kwenye kikao hicho walikubaliana kutotoa taarifa yoyote hadi hapo watakapofikia muafaka, lakini wameshangazwa na kocha huyo kuanza kutoa taarifa kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Chanzo hicho kimesema baadhi ya maswali aliyoulizwa kocha huyo ni kwamba, kwanini hakutoa taarifa mapema, alikwenda wapi na kufanya nini. Maswali hayo imedaiwa alishindwa kuyajibu.

“Baada ya kusimamishwa wiki iliyopita, tulikubaliana tusiweke wazi hadi Kamati ya Nidhamu itakapomaliza kila kitu juu ya jambo hilo, lakini baada ya jana (juzi) anaandika huo ujumbe kwa sababu anafahamu wazi amefanya makosa hivyo, anatafuta huruma ya mashabiki ili aonekane hana kosa.

“Tulimuuliza kwanini aliondoka bila ruhusa, ulikwenda wapi na kufanya nini lakini alishindwa kujibu maswali hayo, hivyo anachokifanya ni kuwaaminisha mashabiki kuwa bodi haiko sahihi.

“Kesho (leo Jumamosi) uongozi utaweka wazi hatima yake na maamuzi yaliyotolewa kwa siku hizi mbili, jana (juzi) tulipokutana naye na leo (jana Ijumaa) tutakutana kujadili kwa mara ya mwisho,” alisema kiongozi huyo

Kuhusu ujio wa kocha mpya ambapo miongoni mwa makocha wanaotajwa ni Lamine N’diaye anayeifundisha Horoya ya Guinea, bosi huyo alisema:

“Kiukweli bado tunaangalia, ni jambo gumu kidogo kwa sababu tupo katikati ya msimu, hivyo kulisema kwa sasa inakuwa vigumu hadi mchakato ukamilike.”

Kuhusu mkataba wa Aussems endapo utavunjwa, alisema kila kitu kitakachoamuliwa basi kitazingatia makubaliano ya mkataba walioingia wakati wanampa mkataba mpya.

Chanzo hicho kilieleza kuwa mbali na hayo yote, lakini kocha huyo hajawahi kutoa taarifa yoyote kitaalamu kama alivyoagizwa kama ajira yake inavyomuelekeza.