Aussems awatega Gadiel, Tshabalala

Muktasari:

Beki huyo wa kushoto aliyeibuliwa kutoka Yanga B, alisema Tsahabalala kuna baadhi ya vitu vya jadi ambavyo huwa anajiongeza pindi anapokuwa uwanjani tofauti na vile

NYOTA wa Simba wanaendelea kujifua jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi yao ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC pamoja na ile ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo ya Msumbiji, huku Kocha Patrick Aussems akiwatega kiaina nyota wake, Gadiel Michael na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Kocha huyo amefichua, mpaka sasa hakuna mchezaji mwenye uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza, kitu ambacho ni kama mtego kwa kina Michael na Mohammed Tshabalala wanaonekana kuwa na ushindani kwenye beki ya kushoto.

Mbali na eneo hilo, lakini hata kwenye nafasi ya kipa Aishi Manula na Beno Kakolanya nako kuna vita nzito sawa na eneo la kati lililojaza viungo wakali ambapo kwa tathmini na Mwanaspoti imebaini kutakuwa na vita kali mbele ya safari.

Kwa kuangalia Tshabalala na Gadiel kila mmoja amekuwa na ubora na udhaifu wake na hasa wakati timu ikifanya mashambulizi ama ikishambuliwa, wote wakikaba vyema na kupiga krosi za mabao, lakini Kocha Aussems alisisitiza hadi sasa hana kikosi cha kwanza.

Kocha huyo aliyeifikisha Simba robo fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita alisema katika kikosi chake hakuna aliyejihakikishia namba, ila watakaofanya vizuri mazoezini na kwenye mechi ndio watakaopata nafasi ya kucheza mara kwa mara. Aussems alisema wachezaji wote ni wazuri ndio maana wamesajiliwa katika timu hiyo, hivyo hakuna mwenye uhakika wa kucheza, lakini kulingana na mechi zilivyokuwa nyingi msimu huu kila mmoja atacheza kama ilivyokuwa msimu uliopita.

“Si rahisi kuzungumzia kiwango cha mchezaji mmoja mmoja, kwangu wote wapo vizuri na ambacho nataka waweze kucheza kitimu ili kufikia malengo ambayo tumejipangia na si kuangalia kucheza kwa ubinafsi,” alisema Aussems.

Kuhusu ushindani uliopo kikosini, Gadiel alisema upo kwa timu yoyote ile na kukutana kwake na Tshabalala ambaye hata kwenye timu ya taifa, Taifa Stars anakutana nao kwake haoni tatizo.

“Kikubwa nitakuwa natimiza majukumu yangu nitakayopangiwa na makocha wote pindi ninapokuwa katika mazoezi na mechi ambazo nitapata nafasi ya kucheza na mwisho wa siku wao ndio wenye jukumu la kuamua nani acheze,” alisema Gadiel.

Naye beki wa zamani wa Yanga, Anwar Awadh alisema kwa muda aliopata kukifuatilia kikosi cha Simba tangu kuanza kwa msimu huu amebaini Tshabalala ni beki mzuri ila amekutana na ushindani wa kutosha kutoka kwa Gadiel ambaye naye ni mzuri.

Beki huyo wa kushoto aliyeibuliwa kutoka Yanga B, alisema Tsahabalala kuna baadhi ya vitu vya jadi ambavyo huwa anajiongeza pindi anapokuwa uwanjani tofauti na vile anavyopewa na makocha wake vinavyoweza kulishawishi benchi la ufundi kumpa nafasi ya kuwa chaguo la kwanza.

“Kiujumla Simba wamefanikiwa kuwa na mabeki wa kushoto bora kwa wakati huu ambao binafsi atakayepata nafasi ya kucheza kulingana na mechi husika ilivyo sina wasiwasi naye, bali naamini atakwenda kufanya kazi alivyoagiwa akihofia kuharibu na kumpa nafasi mwenzake.”