Aussems awakomalia Waarabu

Muktasari:

Mazoezi hayo yalitumia dakika 30 huku ikionekena wazi, Aussems amelenga Simba iwakabili JSS kwa soka la kushambulia kwa haraka huku wakipitisha mipira kwa mawinga.

KAMA JS Saoura ya Algeria walioshuka nchini usiku wa jana kutoka kwao, wanaota kupata ushindi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho Jumamosi kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Simba, basi pole yao.

Unaambiwa Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems amewashtukia mapema na kuanza kuwaundia mkakati wa kuwaliza kabla ya kuwafuata Wakongo wa AS Vita kule Kinshasa wiki ijayo.

Ni hivi. Simba iliyorejea jijini juzi kutoka Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ikiwaacha vijana wao na baadhi ya nyota wa kikosi hicho kumaliza kazi kwenye nusu fainali iliyochezwa leo, walipiga tizi la maana la kuimaliza JSS.

Simba iliyopangwa Kundi D na inayoshiriki hatua ya makundi kwa mara ya pili baada ya awali kucheza 2003, ilijifua kwenye Uwanja wa Boko Veterani huku Aussems akionekana kuwapania Waalgeria hao kwa kuwapa tizi la maana vijana wake. Pascal Wawa na Juuko Murshid wakioneklana walipikwa vilivyo ili kuibeba safu ya ulinzi ya timu hiyo.

Aussems alitumia muda kama nusu saa kuwapigisha vijana wake tizi la kucheza mpira kwa pasi fupi fupi na kisha ndefu, lakini huku akitumia muda mwingi kuwapa kazi nzito Juuko na Wawa ambao watakuwa na majukumu mazito kwa JS Saoura.

Katika mazoezi hayo Mbelgiji huyo alionekana kutumia muda mwingi kuwajenga mabeki hao na wale wa pembeni, Nicholas Gyan na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ waliokuwa wakianzishwa mipira mirefu na kukimbia kupiga krosi.

Krosi za kina Tshabalala na Gyan sambamba na pasi zao za chini za haraka zilikuwa zikilengwa kwa washambuliaji John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi huku Cletous Chama, Haruna Niyonzima na Rashid Juma wakifanya kazi ya kuwafunga Aishi Manula na Deo Munishi ‘Dida’ waliokuwa wakipokezana kukaa langoni.

Mazoezi hayo yalitumia dakika 30 huku ikionekena wazi, Aussems amelenga Simba iwakabili JSS kwa soka la kushambulia kwa haraka huku wakipitisha mipira kwa mawinga.

Mara baada ya kumaliza zoezi hilo, Aussems aliwagawa wachezaji wake katika timu mbili tofauti ya kwanza ikiwa na Wawa, Juuko, Rashid, Mzamiru, Niyonzima, Ndemla na Kagere, huku ya pili ikiwa na kina Kotei, Mkude, Tshabalala, Chama, Bocco, Dilunga, Okwi, Gyan.

Katika mazoezi hayo, Manula na Dida walikuwa wakipambana kuzuia mipira isiingie nyavuni huku Wawa na Juuko wakihakikisha wanakaba hadi kivuli, ambapo tizi hilo lilionekana kumpa mzuka zaidi Aussems, ambaye alikuwa akishangiliwa muda wote na mashabiki waliojitokeza kushughudia.

Mabeki hao wa kati wanaotarajia kuanza mchezo wa kesho walionyesha umakini mkubwa na Aussems, alisema amefanya hivyo ili kutengeneza timu ambayo itaweza kuwazuia JSS akiamini ni moja ya timu ngumu katika kundi lao.

Hata hivyo, alisisitiza kwamba lengo lake ni kuona anavuna alama tatu kabla ya kuwafuata AS Vita kisha kwenda Misri kumalizana na Al Ahly ambao wanatajwa kuwa ni timu tishio kwa sasa kutokana na kufanya usajili wa kutisha.

“Mipango yetu kuwapa raha mashabiki, mechi hizi ni ngumu na lazima tujifue vyema kuhakikisha tunashinda. Tutakuwa nyumbani ni muhimu kupata matokeo mazuri kabla ya kwenda kucheza ugenini. Mashabiki wetu wasiwe na hofu kabisa na waje uwanjani kwa wingi kuwapa hamasa wachezaji kwani, uwepo wao ni muhimu sana kwetu,” alisema Aussems.