Aussems ataondoka, viongozi Simba nanyi mjipime

Muktasari:

Wakati anaondoka kocha huyo ambaye ameipa Simba ubingwa msimu uliopita na kuifikisha robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo walitolewa na TP Mazembe ya DR Congo.

MAPEMA wiki hii kocha wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems amezua taharuki na sintofahamu kwa mashabiki wa Simba kutokana na kuondoka kwake ghafla ingawa yeye aliweka sawa kuwa angerejea kuendelea na ajira yake.

Kwa sasa mashabiki wa soka wamesahau kutimuliwa kwa Mwinyi Zahera aliyekuwa kocha wa Yanga kutokana na mwenendo mbovu wa timu yao, wamegeukia kutaka kujua hatima ya Aussems nini kitafuata juu yake.

Alfajiri ya Jumatatu, Aussems alianza safari ya kuelekea Kipawa ulipo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere akielekea nje ya nchi.

Wakati anaondoka kocha huyo ambaye ameipa Simba ubingwa msimu uliopita na kuifikisha robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo walitolewa na TP Mazembe ya DR Congo.

Taharuki hiyo ilianza kuhusianishwa na mabadiliko ya benchi la ufundi ambapo inadaiwa viongozi wa Simba wapo kwenye mchakato wa kutaka kulifumua ikidaiwa kuwa nusu ya waliopo wataondoka akiwemo Aussems.

Sababu mbalimbali zinaelezwa ambazo zinatajwa kuwa ndizo chanzo cha kumfanya Aussems akalie kuti kavu ikiwemo utovu wa nidhamu kwa wachezaji na timu kucheza chini ya kiwango japokuwa matokeo yao msimu huu wa ligi si mabaya.

Simba ndio wanaoongoza ligi wakiwa na pointi 22 wakiwa wamecheza mechi tisa ambapo wameshinda saba, wametoka sare mmoja wakipoteza mechi moja dhidi ya Mwadui FC.

Tangu kuanza kwa msimu huu, mambo ndani ya benchi la Simba siyo mazuri sana kwani wanajikuta wapo kwenye wakati mgumu kutokana na mwenendo mbovu wa timu yao wakiwa wametolewa mapema katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika tofauti na msimu uliopita.

Matokeo hayo yaliwakatisha tamaa viongozi wa klabu hiyo huku wanachama na mashabiki wao nao wakianza kuingiwa na hofu, ingawa wamewekeza nguvu zaidi kupigania kutetea ubingwa wao.

Aussems ana mkataba na Simba ambao alisaini mara baada ya mkataba wa kwanza kumalizika - mkataba mpya ni wa mwaka mmoja pekee, lakini kwa jinsi mambo yanavyokwenda unaweza kuvunjwa na hapo itategemea makubaliano yalikuwaje kwenye ulipwaji wa uvunjaji wa mkataba huo.

Wakati kocha huyo anaingia ndani ya Simba alimkuta Mrundi Masoud Djuma anakaimu nafasi hiyo, lakini Aussems alishindwa kwenda sawa na msaidizi wake ambapo walilazimika kukaa mezani na kuvunja mkataba wa Djuma kwani Mbelgiji huyo aliwapa masharti viongozi wake kwamba wasipomuondoa basi yeye ataondoka.

Najaribu kufikiria sababu ambayo ilimuondoa Djuma kwamba hakuwa na nidhamu, hakuwa na ushirikiano mzuri na Aussems huku akiwashawishi wachezaji wacheze chini ya viwango ili bosi wake aonekane utendaji wake ni mbovu na atimuliwe apewe nafasi yeye.

Lakini naanza kuhusishanisha hivi sasa tetesi za kutaka kuondolewa kwa kocha huyo ni kutokuwa na ushirikiano mzuri na wenzake kwenye benchi la ufundi, timu haina nidhamu hasa wachezaji kutokuwa na nidhamu, haya mambo ndiyo yaliyomuondoa.

Inatafakarisha kidogo juu ya suala la nidhamu ndani ya Simba linashindikana kukoma kabisa tangu lianze kupigiwa kelele miaka na miaka na ni mara chache linapungua na kurudi hasa kwa wachezaji.

Hii inaonyesha kwamba hakuna mfumo mzuri ambao pia unaweza kumshinda hata Mkurugenzi Mkuu, Senzo Mazingisa ambaye pengine hajazoea mazingira ya soka la Bongo hasa upande wa maisha ya wachezaji jinsi wanavyoishi na viongozi wao.

Senzo akae akijua tu kwamba Simba kuna wachezaji ambao watamsumbua sana na hawaguswi hovyo, kitu ambacho kinawapa jeuri matokeo yake makocha ndiyo hubebeshwa zigo la adhabu kwa kuonekana hawafai bila kuangalia mfumo wao wa uongozi ukoje kwa wachezaji wao.

Hilo ni dogo, timu haionyeshi kiwango bora, pia viongozi wanapaswa kuangalia tatizo limeanzia wapi, je usajili ulifanywa na kocha wao? Maana baadhi ya wachezaji waliosajiliwa inadaiwa haikuwa pengekezo la mwalimu wao zaidi ya Francis Kahata kutoka Gor Mahia ya Kenya.

Ni vyema kama viongozi wa Simba mtaamua kufanya maamuzi basi hata upande wenu muangalie kwa kina kwanini yote haya yanatokea na yanasababishwa na nani.

Kwa maana nyingine yaani mjue chanzo ni nini maana mnaweza kujikuta siku zijazo hata Senzo mtamuona hafai, mtaona ameshindwa kumaliza tatizo la utovu wa nidhamu ambalo analipigia kelele na ameliweka mbele kulipambania limalizike.

Kama Aussems atatimuliwa lazima atakumbukwa kwa mazuri yake ya ndani ya msimu mmoja lakini akiletwa kocha mwingine naye itabidi aingie akijuwa kwamba anakikuta kikosi ambacho si chake, kimetoka kwenye mfumo mwingine hivyo kabla ya kusaini mjulishane kukubaliana kupokea matokeo ya aina yoyote.