Aussems ataka ubingwa wa Simba kwa Singida United

Tuesday May 21 2019

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Patrick Aussems ameitumia salamu Singida United kwa kusema wanaenda Singida kwa lengo la kutangazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 88, watani zao, Yanga wapo nafasi ya pili wakiwa na alama 83 huku wakiwa wamesaliwa na michezo miwili kabla ya msimu kumalizika.

Aussems alisema hawaendi Singida kwa lengo la kutafuta pointi moja ambayo Simba wanahitaji ili kutangazwa kutetea ubingwa wao bali ni kwa ajili ya kutafuta pointi zote tatu za mchezo huo.

“Natamani tuujaze uwanja wao, Jumanne itakuwa siku muhimu kwetu naamini tunaenda kupata pointi tatu ambazo zitatufanya kutetea ubingwa wetu,” alisema kocha huyo.

Akizungumzia kiwango cha safu yake ya ushambuliaji, Aussems alisema imefanya kazi nzuri msimu huu na inastahili pongezi kutokana na idadi ya mabao waliyofunga.

“Najisikia furaha kuona washambuliaji wangu wakifanya kile ambacho wanatakiwa kufanya kwa ufanisi mkubwa, japo kuna michezo huwa wanapoteza nafasi ila naweza kusema kiujumla wamefanya kazi nzuri,” alisema.

Advertisement

Idara ya ushambuliaji ya Simba inajumla ya mabao 52 kati ya 74 ambayo timu hiyo imefunga msimu huu, katika idadi hiyo ya mabao ya mastraika wa wekundu hao wa Msimbazi, Meddie Kagere ambaye ni kinara wa ufungaji amefunga mabao 22.

Mshambuliaji wa Uganda, Emmanuel Okwi na nahodha wa timu hiyo, John Bocco kila mmoja amepachika mabao 15.

Advertisement