Aussems asuka Simba ya mabao tu

Wednesday August 14 2019

 

By Thomas Ng'itu na Olipa Assa

KIKOSI cha Simba kimeendelea na mazoezi yake katika Uwanja wa Gymkhana kwa ajili ya mchezo wa Ngao ya Hisani dhidi ya Azam.

Simba na Azam zitacheza mchezo huo Jumamosi saa moja usiku katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, na tayari ushindani na tambo zimeanza kutikisa mashabiki wake.

Hata hivyo, Mwanaspoti ambalo lilitia timu kwenye mazoezi yaliyofanyika jana jioni, limebaini kuwa kocha Patrick Aussems anatengeneza kikosi cha kuzalisha mabao zaidi.

Katika mazoezi hayo, Aussems aliwapa shughuli moja tu mastraika wake, John Bocco na Meddie Kagere, ambayo ni mbinu za ziada za kuwakimbia mabeki kwa haraka na kupasia nyavuni.

Kagere na Bocco hawakutakiwa kukaa na mipira wanapopokea pasi kutoka kwa viungo akiwataka kugusa mpira mara moja ama mbili kisha kupiga mashuti langoni ambako Benno Kakolanya alikuwa na kazi ya ziada kuokoa.

Hata hivyo, kama ilivyotarajiwa kazi ya kufunga kwenye mazoezi hayo ilifanywa vizuri na Kagere na Bocco na kuzidi kumpa mzuka Aussems.

Advertisement

Pia, shughuli ya kupewa mbinu za ziada ilikuwa kwa viungo na mabeki ambapo kila mmoja alitakiwa kucheza kwa nafasi huku mabeki wakikaba kuanzia juu na wakitengeneza muunganiko ambao washambuliaji kupita walitahitaji kazi kwelikweli.

Vikosi vilikuwa na Santos Da Silva, Pascal Wawa, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Shomari Kapombe, Gerson Fraga, Hassan Dilunga, Deo Kanda na Cletus Chama, Hassan Mlipili, Kennedy Juma, Haruna Shamte, Miraj Athuman, Jonas Mkude na Rashid Juma.

Kwa upande wa kocha wa viungo, Aden Zrane alikuwa na kazi ya kuwaongezea pumzi wachezaji wake akiwafunga vifaa maalumu kama puto huku wakitimua mbio.

MANULA, WILKER WAIBUKA

Kipa namba moja, Aishi Manula na Wilker Da Silva ambao walikuwa majeruhi, jana waliibuka mazoezini licha ya kutoshiriki na wenzao.

Manula, ambaye anasumbuliwa na maumivu ya nyonga yuko nje kwa wiki tatu huku Mbrazil Wilker akisumbuliwa na majeraha ya goti aliyoyapata kwenye mchezo dhidi ya Orlando Pirates kule Afrika kusini.

AUSSEMS AFUNGUKA

Aussems alisema hawana namna zaidi ya kufunga mabao mengi zaidi kwenye mechi za mashindano wakianzia na Azam FC.

Alisema baada ya suluhu dhidi ya UD Songo ya Msumbiji, kwa sasa anajenga kikosi chake ili kuhakikisha wanazalisha mabao mengi wakiwa uwanja wa nyumbani na baadaye kwenye mechi za ligi.

Alisema watatumia mchezo huo dhidi Azam FC kwenye Ngao ya Hisani, ataweka tahadhari kubwa na hatacheza nayo kwa mazoea akiamini wapinzani wao hao wamebadilika.

“Wachezaji wapo sawa wanatamani kuona mechi ya marudio na UD Songo tunapata matokeo ili kufika mbali, mechi yetu na Azam FC itatupima kwani ipo vizuri licha ya kufungwa bao 1-0 na Fasil Kanema ya Ethiopia,” alisema.

Advertisement