Aussems apanga sapraizi Msimbazi

Friday August 23 2019

 

By Olipa Assa

KOCHA Patrick Aussems amepanga sapraizi ya maana kwa mashabiki wa Simba kwenye mechi yao ya Jumapili, akitamba mapema kwamba UD Songo ya Msumbiji wajiandae kuumia tu katika mechi yao ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2019-2020.
Aussems amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwamba tayari amekiandaa kikosi kazi kitakachowapa furaha kwenye mechi hiyo, aliodai ni muhimu kwao kushinda na sapraizi watakayoipata hawataisahau tangu timu yao iwe chini yake katika michuano hiyo.
Kocha huyo amesema hachukulii poa mchezo huo, isipokuwa amekijenga kikosi ambacho ndio silaha yake kubwa ya kutimiza ndoto za kufika mbali kwenye michuano hiyo na ikiwezekana kuvuka hatua walioishia mwaka jana.
Ligi ya Mabingwa Afrika iliopita, Simba ilifika hatua ya robo fainali ambapo ilitolewa na TP Mazembe, akifungwa bao 4-1 ugenini na nyumbani iliruhusu suluhu.
Katika mechi zao tano za awali kabla ya kutinga hatua hiyo, Simba haikupoteza mchezo wowote nyumbani zaidi ya kushinda ikianza kwa kuifunga Mbabane Swallows kwa mabao 4-0, kisha kuinyoosha Nkana Red Devils kwa mabao 3-1, katika makundi iliifunga JS Saoura kwa mabao 3-0, Al Ahly (1-0) na kuinyuka AS Vita kwa mabao 2-1.
"Utakuwa mchezo mgumu, hata hivyo malengo yetu ni ushindi, tunahitaji kusonga mbele kuona tunavuka hatua ambayo mwanzo tulifika, si kazi rahisi ila inahitaji nia ya dhati hakuna kinachoshindikana na mashabiki waje waone kitakachotokea Taifa," alisema.
Aussems alisema wachezaji wapo sawa isipokuwa John Bocco aliyeumia katika mechi dhidi ya Azam FC na atamtumia straika mmoja ambaye ni Meddie Kagere, huku akitumia viungo washambuliaji na mawinga kama kina Deo Kanda, Francis Kahata, Clatous Chama na wengine kumaliza mambo.

Advertisement