Aussems: rekodi ya Tanzania Prisons si tatizo kwetu

Muktasari:

Tanzania Prisons ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu Tanzania Bara hadi sasa

Dar es Salaam.Kocha wa Simba, Patrick Aussems amesema rekodi ya wapinzani wao Tanzania Prison katika Ligi Kuu Tanzania Bara wala si tatizo kwao.

Akizungumza baada ya mazoezi ya leo asubuhi, Aussems alisema Prison ndio timu ambayo haijapoteza mechi yoyote mpaka sasa, lakini wametoka suluhu nyingi.

"Wanaingia katika mchezo huu wakiwa na rekodi nzuri, lakini kwetu wala siyo tatizo tumejipanga kufanya vizuri dhidi yao," alisema Aussems.

"Tumepata muda wa kuwafuatialia ambavyo wanacheza na kwangu tumeandaa timu kulingana na wapinzani wetu walivyo.

"Kuna baadhi ya wachezaji watakosekana katika safu ya ushambuliaji, lakini kuna ambao watacheza na kuziba mapengo yao vizuri na tukapata matokeo ya ushindi," alisema.

Naye Kocha wa Prison, Mohamed Rishard 'Adolf' alisema unapocheza na timu kama Simba si muda wa kuangalia matokeo ya nyuma.

"Maandalizi yetu kiujumla ni mazuri na leo siku ya mwisho tulifanya mazoezi ya kucheza zaidi na hili ndio ambalo tutakwenda kulifanya katika mechi ya kesho," alisema Adolf.

Timu hizo mbili zimekutana mapema leo kwenye Uwanja wa Uhuru utakaotumika kwa mchezo wa kesho.

Prison ilikuwa wa kwanza kufika uwanjani hapo saa 2, asubuhi na kufanya mazoezi mpaka saa 4:00 asubuhi.

Simba wao walifika uwanjani hapo saa 3:53 asubuhi na kulazimika kusubiri kwanza Prison wamalize mazoezi ili na wao ndio waingie uwanjani.

Wakati Simba wanaingia na basi lao kubwa uwanja wa Uhuru, basi la Prison nalo lilingia kwenda kuchukua wachezaji na aalipomaliza mazoezi waliondoka.

Wakati Prison wanamaliza mazoezi baadhi ya wachezaji na makocha wao walisalimiana na wachezaji na benchi la ufundi kwa ujumla.

Baada ya Prison kuondoka wachezaji na benchi la ufundi la Simba waliingia uwanjani na kuanza kufanya mazoezi yao mbalimbali huku mvua ikiwa inanyesha ingawa si sana.