Aussems: Neema inakuja Simba tulieni

Friday August 10 2018

 

By OLIPA ASSA

Dar es Salaam. MASHABIKI wa Simba, wametoa somo kwa kocha wa kikosi hicho, Mbeligiji Patrick Aussems hii ni baada ya jana kujaza uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, wakati wa tamasha la Simba Day, jambo lililomfanya atamke kuwa ana deni kubwa katika ligi inayokuja.

Aussems alisema nyomi ya mashabiki aliyoiona jana wakati wakitambulishwa rasmi, maalumu kwa msimu ujao ilimpa taswira ya kujua Simba ni timu ya aina gani Tanzania.

"Nimepata picha nzima kujua mashabiki wanahitaji nini kwa benchi la ufundi na wachezaji kwa ujumla, najiona kama mwenye deni kwao, kikubwa wajue wana timu nzuri inayoweza kufanya kitu cha kuwaletea tabasamu.

"Karibia tunaanza msimu mpya, basi nitoe wito kwao kwa namna ambavyo walijitokeza katika tamasha la Simba Day, waendelee kufanya hivyo kwenye ligi kwani hatutawaangusha,"anasema.

Mbali na hilo alizungumzia maandalizi kwa ujumla kwamba wamejiandaa kikamilifu na kudai kuwa ana kikosi kipana, kinachompa uhuru wa nani amtumie na kwa wakati gani.

"Nina wachezaji ambao wanaweza wakafanya kazi nzuri na yenye kuleta tija, kuhusu kutoka sare na Asante Kotoko ya Ghana, ni kwa sababu ya kutoka kwenye maandalizi ya msimu, ila ligi ikianza basi kazi yetu itashuhudiwa na wengi kuwa ni bora,"anasema.

 

Advertisement