Aussems, Mayanja, Ndayiragije washindwe wao tu, ila Zahera kutachimbika

Muktasari:

Timu nne za Tanzania zikiwa na makocha wanne wa kigeni zitaiwakilisha nchi katika michezo ya kimataifa mwishoni mwa wiki, tatu zikicheza nyumbani na moja ugenini.

Dar es Salaam. Makocha Patrick Aussem wa Simba, Ettienne Ndayiragije wa Azam na Jackson Mayanja wa KMC wanamewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kulinganisha na Mwinyi Zahera wa Yanga katika michezo ya kimataifa ya wiki hii.

Timu nne za Tanzania zikiwa na makocha wanne wa kigeni zitaiwakilisha nchi katika michezo ya kimataifa mwishoni mwa wiki, tatu zikicheza nyumbani na moja ugenini.

Mayanja baada ya kuiongoza KMC kupata suluhu ugenini atakuwa na kazi moja ya kuhakikisha anashinda mchezo wa Ijumaa hii dhidi ya AS Kigali kwenye Uwanja wa Taifa.

 Kocha Mayanja tangu amerejea toka Kigali amekuwa akifanya mazoezi ya upigaji penalti katika kuhakikisha anashinda mchezo huo hata baada ya dakika 120.

Naye Kocha Ndayiragije atakuwa na kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha Azam inashinda mechi yake dhidi ya Fasil Kenema ya Ethiopia Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Ndayiragije amepoteza mechi mbili dhidi ya Kenema na ile Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, lakini akiwa na mabadiliko kidogo kati kikosi chake kutoka kile kilichocheza Ethiopia kwa kuwaanzisha washambuliaji wawili ambao na kufanikiwa kupata mabao mawili.

Pamoja na kipigo cha mabao 4-2, bado Mrundi huyo amefanikiwa kwa kupata mabao hayo mawili katika mechi ya mashindano tangu alipochukua kikosi hicho, hivyo kucheza nyumbani itakuwa ni faida nyingine kwake.

Katika Ligi ya Mabingwa kocha Mwinyi Zahera atalazimika kufanya kazi ya ziada kutegeneza kombinesha pamoja na uchezaji wa kitimu wa kikosi chake Jumamosi hii dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

Yanga imefanya usajili mkubwa wa nyota 13, lakini tatizo linalowasumbua kwa sasa ni wachezaji kukosa muunganiko jambo linalowaweka katika mazingira magumu kuelekea mchezo huo dhidi ya Rollers.

Akizungumzia baada ya ushindi wake dhidi ya AFC Leopars, kocha wa Yanga, Zahera alisema matokeo hayo hayakuwa ya kiufundi pamoja na kwamba tumeshinda.

"Tumepata matokeo, lakini bao halikuwa la kiufundi bali la bahati, tumecheza katika uwanja mbovu, si Arusha tu hata Moshi (walicheza na Polisi Tanzania na kufungwa 2-0), hazikuwa mechi za kiufundi," alisema Zahera.

Hata hivyo Zahera alijipa matumani kwa kusema watakapokuwa Botswana watacheza soka la kiufundi kwani hawatarajii uwanja uwe mbovu kule na watacheza soka la mipango na kusaka matokeo.

Wakati Zahera akilia mazingira mabovu ya maandalizi yake, hali ni tofauti kwa Simba ambayo inalingia kikosi chake na uzoefu.

Simba inawakiribisha UD Songo ya Msumbiji Uwanja wa Taifa ikijivunia ushindi wake wa mabao 4-2 dhidi ya Azam, pamoja na rekodi yake nzuri ya kushinda mechi zake wakiwa nyumbani katika mashindano ya Afrika.

Kocha Aussems anajivunia kiwango bora cha kiungo Msudani, Shariff Shiboub, mshambuliaji Meddie Kagere na kiungo Cletous Chama itakuwa silaha tosha ya kutimiza ndoto yao ya kusonga mbele.

Wakizungumzia nafasi ya timu za Tanzania katika michezo hiyo makocha mbalimbali wamesema Simba, KMC na Azam zitakazocheza nyumbani zinafasi nzuri kulinganisha na Yanga itakayokuwa ugenini pia kiwango chake bado hakiridhishi.

Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi amewataka Yanga kujilipua ugenini kwa kucheza soka la kushambulia na kamwe wasithubuti kujilinda.

"Ukiingalia Yanga na wachezaji wengi wapya karibu 10 hivyo hawawezi kucheza kitimu kwa muda mfupi hivyo kwa sababu wamekutana wachezaji kutoka nchini na klabu zinazotumia mifumo tofauti.

"Ninachowashauri ni kwamba huko ugenini washambulie kutoka dakika ya kwanza, wasiende na mfumo wa kujilinda utawagharimu kwani ukiangalia ni kama hawana cha kupoteza kwa sababu kosa walilofanya ni kuwaruhusu wapinzani wao kupata bao Dar es Salaam.

"Kwa upande wa Simba wana nafasi ya kushinda kwa asilimia 70 ya wachezaji wao ni wale wale na wameongeza kidogo tu hivyo ushirikiano uwanjani utawabeba kama ilivyo kwa Azam ambayo licha ya kwanza wameanza hayo mashindano kwa kupoteza lakini bado nawapa nafasi. Pia hata KMC imesajili wachezaji wazuri na ile suluhu ya ugenini itawawasaidia kufanya vizuri nyumbani," alisema Mwambusi.

Naye kocha wa Namungo FC, Mrundi Hitimana Thierry  alisema anaipa nafasi Simba kushinda mchezo huo kwani tayari wanaujua uzuri wa mashindano hayo huku akisema mechi ya Yanga itakuwa ngumu.

"Simba wameshaonja utamu wa Ligi ya Mabingwa Afrika wanajua vizuri nini wanafanya, pia wamejitahidi kusajili na wachezaji wao wengi bado wako kikosini,”alisema Hitimana.

Hitimana alisema Azam wanatakiwa kuhakikisha hadi mapumziko wanaongoza hata bao moja ingawa kwenye mpira hata kpindi cha pili unafunga, lakini muhimu wazingatie kufunga mabao ya mapema ili yawapunguze presha.

“Yanga yenyewe katika mechi ya kwanza ilijitahidi kidogo kipindi cha pili na nafikiri kinachowagharimu ni kwamba ina wachezaji wengi wapya, lakini kosa kubwa walilofanya ni kuwaruhusu wageni kupata bao kwani kule wanaweza kupata tabu kwa sababu wapinzani wao Township Rollers ni timu inayoonekana imekaa muda mrefu na wanacheza kitimu, lakini wapambane kwani kwenye soka lolote linaweka kutokea"alisema Hitimana.