Aubameyang amhakikishia Mkhitaryan ubingwa Europa Ligi

Friday May 24 2019

 

London, England. Mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang amemhakikishia Henrikh Mkhitaryan tena kwa msisitizo kwamba Arsenal inakwenda kushinda ubingwa wa Europa League katika fainali yao dhidi ya Chelsea huko mjini Baku.

Mkhitaryan hatakuwapo kwenye fainali hiyo itakayopigwa Azerbaijan kutokana na tofauti za kisiasa zilizopo baina ya nchi hiyo na yake ya Armenia, hivyo kumekuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wake.

Kitendo cha kupeleka fainali hiyo mjini Baku kimekuwa kikisogolewa vikali hasa baada ya klabu hizo mbili za London, Chelsea na Arsenal kila moja kupewa tiketi 6,000 tu na mashabiki wamedaiwa kukabiliwa na changamoto kubwa kwenye kupata kibali za kuingia nchi humo kwenda kutazama mechi.

“Tufahamu hii ni aibu kubwa sana, lakini lazima tuheshimu uamuzi wake," alisema Aubameyang akimzungumzia Mkhitaryan.

"Sio kitu rahisi kabisa kwa upande wake kushindwa kwenda kwenye fainali kisa tu matatizo ya kisiasa. Ni aibu, lakini sisi tumepata hamasa zaidi ya kwenda kushinda. Kila mtu anataka kurudi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na huo umekuwa mpango wetu tangu mwanzo wa msimu.”

Kipa Petr Cech, ambaye kwenye fainali hiyo atacheza dhidi ya klabu yake ya zamani alizungumzia jambo hilo na kusema: “Siasa na michezo siku zote havipaswi kuwekwa pamoja. Michezo inaunganisha watu, hivyo ilipaswa kutumika kuondoa matatizo.

Advertisement

“Tunapochagua sehemu za kucheza mechi za fainali tunapaswa kutazama mambo kama haya, ichezwe kwenye sehemu ambayo kila mtu atakwenda bila ya kuwa na matatizo yoyote.”

Advertisement