Aubameyang aanza tambo Arsenal

Muktasari:

Kinara wa mabao Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang amesema ana matumaini klabu hiyo itakuwa tishio katika mashindano ya Ligi Kuu England msimu huu.

London, England. Mshambuliaji wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang amsema wako tayari kupigania ubingwa katika Ligi Kuu England msimu huu.

Aubemeyang alisema Arsenal imejiandaa kutoa upinzani katika Ligi Kuu baada ya kuanza vyema katika mechi mbili za mashindano.

Mchezaji huyo alisema wamejiandaa kushinda kila mchezo baada ya kuilaza Newcastle United bao 1-0 kabla ya kuigagadua Burnley mabao 2-1.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Gabon, alisema matokeo hayo ni salamu kwa wapinzani msimu huu.

Awali, Kocha wa Arsenal, Unai Emery alisema wataishangaza England msimu huun kwa kuwa ana kikosi bora.

“Nadhani tangu mwanzo nilisema mapema tumefanya usajili mzuri na utakuwa na manufaa kwetu,”alisema Aubameyang.

Nyota huyo alisema msimu uliopita Arsenal haikuwa mbali kukata tiketi kucheza Ligi ya  Mabingwa Ulaya, lakini msimu huu ni zamu yao.

‘Najua lolote linaweza kutokea mbele ya safari lakini ukweli ni kwamba tunataka ubingwa msimu huu,”aliongeza kinara huyo wa mabao Arsenal.

Aubameyang alifunga mabao yote ya ushindi katika mechi hizo mbili na matumaini yake ni kuipa mafanikio klabu hiyo yenye Makao Makuu Emierates.