Atletico Madrid inavyotisha kwa Mastraika wa nguvu

LONDON, ENGLAND. STRAIKA, Diego Costa ametania kuhusu kombinesheni yake na Luis Suarez itakavyokuwa huko Atletico Madrid, kwamba mmoja atakuwa anang’ata na mwingine anapiga mateke.

Washambuliaji hao watukutu watakuwa pamoja Wanda Metropolitano baada ya Suarez kukamilisha uhamisho wake wa Pauni 5.5 milioni akitokea Barcelona wiki iliyopita.

Juzi Jumapili, Suarez alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na uzi wa Atletico Madrid wakati alipotokea benchi kuchukua nafasi ya straika mwenzake, Diego Costa.

Kwenye mechi hiyo, Suarez alifunga mara mbili na kuasisti mara moja kwa dakika 19 tu alizokuwa ndani ya uwanja wakati Atletico Madrid ilipoichapa Granada 6-1.

Akizungumza baada ya mechi hiyo kuhusu ujio wa Suarez, Costa alisema: “Safi sana. Mmoja anang’ata na mwingine anapiga mateke.”

Ujio wa Suarez kwenye kikosi cha Atletico Madrid unaorodhesha idadi ya washambuliaji wa kati matata kabisa waliowahi kutokea kwenye soka la dunia. Hii hapa, orodha ya mastraika matata kabisa waliotamba na Atletico Madrid kabla ya Suarez kutua kwenye klabu hiyo ya Wanda Metropolitano.

11.Joao Felix

Mabao: 9

Mechi: 36

Bado mapema, lakini Joao Felix ni mmoja wa washambuliaji wa kati waliopata nafasi ya kukipiga kwenye kikosi cha Atletico Madrid. Staa huyo wa Kireno alitua Atletico kwa pesa nyingi, wakati miamba hiyo iliponasa huduma yake kwenda kuchukua mikoba ya Antoine Griezmann. Felix amefunga mabao tisa katika mechi 36 alizotumikia timu hiyo huku akiaminika kwamba bado ana safari ndefu ya kuthibitisha ubora wake kwenye kutikisa nyavu kutokana na kuwa na umri mdogo.

10.David Villa

Mabao: 15

Mechi: 47

Staa, David Villa aliondoka Barcelona kwenda kujiunga na Atletico Madrid mwaka 2013. Hiki anachokifanya Suarez ni marudio tu ya wakali wengine waliowahi kuhama kutoka Nou Camp kwenda Atletico Madrid. Kwenye kikosi cha Atletico Madrid, Villa alionyesha ubora mkubwa ambapo alifunga mabao 15 katika mechi 47 na alifanya mambo makubwa kabisa wakati kikosi cha Diego Simeone kilipofika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kubeba ubingwa wa La Liga.

9.Fernando Torres

Mabao: 129

Mechi: 404

Staa Fernando Torres alikulia kwenye kikosi cha Atletico Madrid. Alitamba akiwa na miamba hiyo kabla ya kutimkia zake Liverpool, Chelsea, AC Milan na baadaye kurudi tena Atletico Madrid. Huduma yake kwenye kikosi cha Atletico siku zote itakuwa yenye kumbukumbu nzuri kwa straika huyo Mhispaniola ambapo alifunga mabao 129 katika mechi 404 alizochezea miamba hiyo ya Wanda Metropolitano. Uwezo wake wa kufunga ulimfanya Torres kuwa mmoja wa washambuliaji wa kati hatari zaidi wanaposogelea goli la timu pinzani.

8.Alvaro Morata

Mabao: 22

Mechi: 61

Straika, Alvaro Morata ni moja ya washambuliaji wa kati hodari kabisa waliopita kwenye kikosi cha Atletico Madrid. Staa huyo Mhispaniola alipita pia kwenye vikosi vya Real Madrid, Juventus na Chelsea - mahali ambako alitengeneza jina lake na kuwa juu. Licha ya kwamba Morata hakuwa mkali sana akiwa na jezi za Atletico, lakini bado amefunga mabao 22 katika mechi 61. Hata kuwapo msimu huu kwenye kikosi hicho ikiwa amerudi zake kuichezea Juventus kuongoza kwenye fowadi sambamba na supastaa wa Kireno, Cristiano Ronaldo waliyekuwa pamoja Madrid.

7.Diego Costa

Mabao: 81

Mechi: 209

Straika, Diego Coast alikuwapo Atletico akaondoka na sasa amerudi tena kwenye kikosi hicho. Tangu aliporudi akitokea Chelsea, Costa amefunga mabao 17 katika mechi 74 na bado anaendelea kutikisa nyavu. Hakuna anayebisha kwamba Costa alikuwa kwenye kiwango bora sana msimu wa 2013/14, wakati alipofunga mabao 36 katika mechi 52 na kuifikisha Atletico kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo walifungwa kwenye mchezo huo wa fainali na mahasimu wao Real Madrid, huku straika huyo akilazimishwa kuchezwa kwa dakika 10 za mwisho akiwa majeruhi.

6.Sergio Aguero

Mabao: 101

Mechi: 234

Akitajwa kuwa mmoja wa mastraika hatari kabisa kwenye soka la kisasa, Sergio Aguero anayetamba huko Manchester City, aliwahi kukipiga na kutamba akiwa na Atletico Madrid. Aguero alionyesha kuwa hatari huko Atletico akiwa bado kijana, ambapo alifunga mabao 101 katika mechi 234 kabla ya kwenda Man City, ambako ameweka rekodi ya kuwa kinara wa mabao wa muda wote katika kikosi hicho cha Etihad. Kwa kasi ya Muargentina huyo kwenye kufunga mabao lilikuwa suala la kawaida kwa Man City kufungua pochi na kunasa huduma yake na tangu atue England amewasaidia wababe hao kubeba Ligi Kuu England mara kibao.

5.Mario Mandzukic

Mabao: 20

Mechi: 43

Halitakuwa jambo zuri kumwondoa Mandzukic kwenye orodha ya mastraika wa nguvu kabisa waliowahi kutokea kwenye kikosi cha Atletico Madrid. Suala la kufunga halijawahi kuwa tatizo kwa mshambuliaji huyo, ambapo katika mechi 43 tu alizocheza Atletico, alifunga mabao 20. Kilichomwondoa mapema kwenye kikosi hicho ni matatizo yake binafsi na kocha Diego Simeone, huku msimu huo kwenye ligi alifunga mabao 12, akishika namba tano kwenye orodha ya wafungaji bora kwenye La Liga kwa msimu husika.

4.Diego Forlan

Mabao: 96

Mechi: 196

Straika, Diego Forlan hakuna mahali ambako alicheza soka la kiwango bora kabisa ndani ya uwanja zaidi ya alivyokuwa Atletico, ambapo hata alipokuwa hayupo kwenye ubora wake, alifunga mabao 23. Staa huyo wa zamani wa kimataifa wa Uruguay, alinyakua tuzo ya Pichichi na Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya baada ya kufunga mabao 32 katika msimu wa 2008/09 na alikwenda kubeba Kiatu cha Dhahabu cha Kombe la Dunia 2010, kwa wakati huo akiwa akiichezea kikosi cha Atletico.

3.Antoine Griezmann

Mabao: 133

Mechi: 257

Kwenye upande wa mchezaji aliyefanya mambo matata ndani ya uwanja kama mchezaji binafsi, Griezmann alikuwa hatari zaidi, alikaribia hata kuwapa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya miamba hiyo ya Madrid. Bila ya kujali kwamba alikosa mkwaju wake wa penalti kwenye fainali, Griezmann bado mchango wake ulithaminika na kushika namba tatu kwenye Ballon d’Or kwa nyakati zake alizokuwa Atletico na hajawahi kufeli kufunga mabao 20 kwa misimu mitano mfululizo.

2.Jimmy Floyd Hasselbaink

Mabao: 33

Mechi: 43

Kabla ya staa wa Kidachi, Jimmy Floyd Hasselbaink kuja kufanya kweli kwenye kikosi cha Chelsea kwenye Ligi Kuu England, alifanya mambo yake huko Atletico Madrid msimu wa 1999/2000. Kwa msimu wake mmoja tu aliokuwa na wakali hao, Hasselbaink alionyesha kuwa ni moto wa kuotea mbali, wakati alipofunga mabao 24 kwenye La Liga pekee, huku mabao saba akifunga kwenye michuano ya Ulaya na kuivutia Chelsea, huku akifunga mara 33 katika mechi 43.

1.Radamel Falcao

Mabao: 70

Mechi: 91

Mitaa ya Madrid haitasahau jina la ‘El Tigre’ kwa lile alilofanya kwenye La Liga wakati alipoing’arisha Atletico Madrid mbele ya masupastaa wa nguvu, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo. Wakati Manchester United na Chelsea zikishindwa kupata huduma bora kutoka kwa Falcao, staa huyo alikuwa moto Vicente Calderon, ambapo katika mechi 91 alizocheza, alifunga mabao 70.

...