Aston Villa A-Z Chama jipya la Samagoal

KWA sasa maskani ya nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta ni Birmingham nchini Uingereza na sio tena Genk huko Ubelgiji ambako alikaa kwa miaka minne akitokea Lubumbashi alikokuwa akitesa na TP Mazembe ya DR Congo.

Baada ya kufuzu vipimo vya afya, Samatta kwa sasa ni mchezaji rasmi wa Aston Villa ambayo wamepita mastaa kibao ambao wanafanya vizuri katika klabu mbalimbali nchini humo akiwemo James Milner aliyepo Liverpool, Ashley Young aliyekwenda Inter Milan akitokea Manchester United na Christian Benteke anayekipiga pale Crystal Palace F.C.

Samatta ni bunduki mpya ambayo imewekwa katika mtutu wa Kocha Dean Smith aliyekuwa na ndoto ya kufanya kazi na mshambuliaji huyo wa Kitanzania tangu majira ya joto yaliyopita, lakini Genk waligoma kumwachia kutokana na ushiriki wao katika Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Mbali na tatizo la ushambuliaji walilonalo Aston Villa msimu huu, pia Samatta anatazamwa kama mchezaji sahihi ambaye atazipa pengo la Mbrazil Wesley ambaye amepata majeraha atakayekosekana hadi mwishoni mwa msimu.

Chama jipya la Samatta lina historia ya kipekee nchini humo, ikizingatiwa kwamba katika benchi la ufundi, yupo pia beki hodari wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya England, John Terry.

HISTORIA YAO

Aston Villa ilianzishwa Machi 1874 na wanachama wa Villa Cross Wesleyan Chapel, Handsworth ambayo ni sehemu ya mji wa Birmingham. Waanzilishi wa Aston Villa ni Jack Hughes, Frederick Matthews, Walter Price na William Scattergood.

Villa walikuwa miongoni mwa klabu wanachama waanzilishi wa Ligi Kuu England mnamo 1992, na walimaliza msimu huo wakiwa nafasi ya pili nyuma ya Manchester United anayoishabikia Samatta.

Villa pia wamewahi kufika fainali ya Kombe la FA iliyopigwa mwaka 2000, lakini walipoteza katika mchezo huo dhidi ya Chelsea kwa bao 1-0 katika uwanja wa zamani wa Wembley.

UWANJA WA NYUMBANI

Uwanja wa nyumbani wa Aston Villa ni Villa Park ambapo miaka ya nyuma kuanzia 1874 hadi 1876 waliutumia Uwanja wa Aston Park na 1876 hadi 1897 walichezea michezo yao ya nyumbani kwenye Uwanja wa Wellington Road.

Villa Park una uwezo wa kuingiza watazamaji 42,785 na cha kushangaza ni kuwa una rekodi ya kuingiza watazamaji 76,588.

MMILIKI WAO

Baada ya Aston Villa kupanda Ligi Kuu England msimu wa 2017-18 huku ukata ukitawala ndani ya klabu hiyo, hali hiyo ilimfanya mmiliki Tony Xia kutafuta uwekezaji zaidi.

Mnamo Julai 20, 2018 ilitangazwa kuwa kikundi cha NSWE, kampuni ya Misri inayomilikiwa na bilionea wa Misri Nassef Sawiris na bilionea wa Amerika Edeni Edens walikuwa wanawekeza katika klabu hiyo.

Walinunua hisa ya umiliki wa asilimia 55 kwenye klabu hiyo ya Aston Villa, na Sawiris alichukua jukumu la kujiteua kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo akipita bila pingamizi.

Agosti 9, 2019 siku ambayo Aston Villa ilirejea Ligi Kuu England ilitolewa taarifa kuwa sehemu ya uwekezaji wa Recon Group ilikuwa imenunuliwa, hivyo Dk Tony Xia hakuwa na hisa tena ndani ya klabu.

UHUSIANO NA JAMII

Mnamo Septemba 2010, Aston Villa ilizindua mpango katika uwanja wa villa unaoitwa Villa Midlands Foods (VMF) ambapo klabu hiyo itatumia miaka miwili kuwapa wanafunzi mafunzo.

Klabu ya Aston Villa imekuwa ikishirikiana vizuri na Halmashauri ya Jiji la Birmingham. Klabu hiyo itafungua mgahawa katika mji wao na sehemu ya jamii ya eneo hilo itapata nafasi ya kufanya kazi ndani ya mgahawa huo ambamo vitakuwa vikipikwa vyakula mbalimbali.

WAPINZANI WA VILLA

Wapinzani wa Aston Villa ni Birmingham City, ingawa kihistoria West Bromwich Albion wamekuwa wapinzani wakubwa wao wakubwa kwa mujibu wa utafiti ambao ulifanywa 2003.

MATAJI

Kipindi hicho Ligi Kuu England ikiitwa Ligi Daraja la Kwanza, Aston Villa walitwaa mataji saba ya ligi hiyo katika misimu ya 1893–94, 1895–96, 1896–97, 1898–99, 1899–1900, 1909–10 na 1980–81.

Upande wa Kombe la FA nchini humo chama hilo jipya la Samatta limebeba pia mataji saba ambapo ilikuwa katika msimu ya 1886–87, 1894–95, 1896–97, 1904–05, 1912–13, 1919–20 na 1956–57.

Aston Villa sio chama la kizembe kwani linamiliki taji moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya - kipindi hicho ligi hiyo ilikuwa ikiitwa Kombe la Ulaya, walifanya maajabu hayo msimu wa 1981 hadi 1982.

NEMBO YA KLABU

Wamepita wachezaji wengi Aston Villa huku wengine wakiwa wametangulia mbele za haki kwa mujibu wa mashabiki wa klabu hiyo ambao walipiga kura. Hawa ndio wachezaji wao bora kuwahi kutokea katika klabu hiyo: Gordon Cowans, Eric Houghton, Brian Little, Dennis Mortimer, Stiliyan Petrov, Ron Saunders, Peter Withe, Paul McGrath, Peter McParland, Charlie Aitken, William McGregor, George Ramsay na Billy Walker.