Asitishiwa Mkataba

Muktasari:

HAKUNA kificho tena ndoa ya Simba na Kocha Mrundi Masoud Djuma haipo baada ya mabosi wa klabu hiyo kumsitishia mkataba wake uliosaliwana mwaka mmoja kati ya miwili waliyoingia naye Oktoba mwaka jana.

WATETEZI wa Ligi Kuu Bara, Simba jana walianza rasmi maisha bila ya Kocha Msaidizi wao, Masoud Djuma ambaye amesitishiwa mkataba wake na klabu hiyo, kwa kuipiga African Lyon kwa mabao 2-1 katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo.

Ingawa mabosi wa Simba tangu juzi Ujumaa mara baada ya kikao chao cha faragha na kocha huyo kutoka Burundi walifanya siri, lakini usiku wa jana ilithibitishwa Masoud amesitishiwa mkataba wake rasmi ndani ya klabu hiyo.

Kocha huyo aliyetambulishwa kwa mbwembwe Oktoba 19 mwaka jana kuchukua nafasi ya Jackson Mayanja, alikuwa na mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo, huku akiutumikia kwa mwaka mmoja hadi juzi kabla ya kusitishiwa.

Mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo (jina kapuni) alilithibitishia kuwa, Masoud sio mali ya Simba na kwamba anajiandaa kuondoka nchini leo kuelekea kwao wakati akisubiri mafao yake ya kusitishiwa mkataba huo.

“Ni kweli Kocha Masoud amesitishiwa mkataba wake klabu na huenda akaondoka kesho (leo) Jumapili kwenda kwao, hata hivyo mtafute Rais (Salim Abdallah ‘Try Again’) ndiye anayeweza kuliweka hili hadharani kwani kila kitu kipo kwake,” alisema Mjumbe huyo.

Kuonyesha maisha ya Masoud Msimbazi yamefikia mwishoni, katika mechi ya jana dhidi ya Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, hakuwepo kabisa uwanjani wala kwenye orodha ya benchi la ufundi la klabu hiyo. Hata hivyo, Mwanaspoti lilimsaka Try Again ambaye alisema yapo mambo kadhaa yamekuwa yakitokea juu ya kocha huyo ila taarifa rasmi ya kuachana naye itatangazwa rasmi. “Ana mkataba wa miaka miwili kama tutavunja mkataba wake basi atalipwa fidia zake zote anazostahili, ila subirini mtatangaziwa rasmi,” alisema Try Again kabla ya mechi.

Kusitishiwa mkataba kwa Masoud kumemaliza fununu za muda mrefu zilizokuwapo kwa kile kilichokuwa kikielezwa haivi na Kocha Mkuu, Patrick Aussems na katika mechi tatu za mkoani Mrundi huyo aliachwa katika msafara na kubakishwa Dar es Salaam.

Masoud alikuwa akituhumiwa kuwagawa wachezaji na mashabiki ambao walikuwa wakimzimikia kwa uhamasishaji wake na matokeo aliyoyapata wakati akikaimu ukocha mkuu baada ya Mcameroon Joseph Omog na Pierre Lechantre raia wa Ufaransa kutimuliwa.

Tangu asubuhi ya jana Masoud alisakwa kwenye simu lakini ilikuwa ikiita bila kupokewa.

Kichuya, Okwi

Katika mchezo wa jana Simba ilijiongezea pointi tatu baada ya kuinyoa African Lyon kwa mabao 2-1, yaliyowekwa nyavuni na Shiza Kichuya na Emmanuel Okwi yakiwa mabao yao ya kwanza kwa nyota hao, huku Haruna Niyonzima akicheza kwa mara ya kwanza msimu huu.

Kichuya alifuta ukame wa siku 222 sawa na miezi 7 na siku 10 tangu alipofunga mara ya mwisho Februari 26 wakati Simba ikiitumbua Mbao FC kwa mabao 5-0 kwa kupachika wavuni bao dakika ya 9 kabla ya Okwi naye kufunga bao la pili dakika ya 48.

Bao hilo la Okwi lilimaliza gundu la siku 153 sawa na miezi mitano kamili kwa straika huyo raia wa Uganda tangu afunge bao lake la mwisho na la pekee katika mchezo wao dhidi ya Ndanda FC uliopigwa Mei 6, 2018 jijini Dar es Salaam.

Lyon ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 62 kwa shuti kali la mbali na Awadh Juma.

Jana pia ilishuhudiwa Niyonzima akicheza kwa mara ya kwanza baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Cletus Chama katika kipindi cha pili, huku akionekana umahiri wake ni uleule kama wa zamani licha ya kuwa nje kwa sababu ya majeraha. Ushindi huo umeifanya Simba kufika pointi 14 na kuchupa hadi nafasi ya nne kutoka ya 10 walikuwapo baada ya matokeo ya jioni ya mechi nyingine, ambapo Singida United iliinyoa Ndanda kwa mabao 3-1 Uwanja wa Namfua, huku Mbeya City ikitaka katika mechi ya Mbeya Derby dhidi ya Prisons kwa kushinda 2-1, huku Mtibwa Sugar na KMC zikifungana bao 1-1 na Kagera Sugar na Ruvu Shootingi zikitoka suluhu mjini Bukoba.

IMEANDIKWA NA KHATIMU NAHEKA NA MWANAHIBA

RICHARD