Asamoah Gyan ajitoa AFCON 2019

Muktasari:

  • Asamoah mwenye umri wa miaka 33, ameitumika Ghana kwa miaka 16 kuanzia 2003 akiifungia jumla ya mabao 51 katika mechi 106 za mashindano mbalimbali

BAADA ya kucheza awamu saba za mashindano ya soka ya Mataifa ya Afrika (AFCON), mshambuliaji wa Ghana, Asamoah Gyan hatoshiriki fainali za mwaka huu zitakazofanyika Misri.

Hiyo inafuatia uamuzi wake wa kujiondoa kwenye kikosi cha awali cha Ghana ‘Black Stars’ kinachojiandaa na fainali hizo na kustaafu moja kwa moja kuichezea timu hiyo aliyotangaza mwishoni mwa wiki iliyopita.

Gyan amechukua uamuzi huo kwa kile kinachoonekana kukerwa na uamuzi wa kocha Kwesi Appiah kumvua kitambaa cha unahodha na kumpa mshambuliaji wa Fenerbahce, Andre Ayew.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu za Sunderland na Al Ain anaona uamuzi wa kumvua kitambaa cha unahodha kama dharau kwake jambo lililomfanya aachane rasmi na timu hiyo.

“Siwezi kujionyesha kuwa nina furaha kwani nitakuwa ninajiumiza mwenyewe kihisia na kisaikolojia. Nimetumikia timu ya taifa kwa moyo mkunjufu na nimejitolea kwa kila hali,” aliandika Asamoah kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Asamoah mwenye umri wa miaka 33, ameitumika Ghana kwa miaka 16 kuanzia 2003 akiifungia jumla ya mabao 51 katika mechi 106 za mashindano mbalimbali