Arusha United waonyesha ubabe wao kwa AFC

Muktasari:

Ushindi wa Arusha United unawaweka kileleni mwa Kundi B ikiwa na pointi 7 baada ya kuwafunga Rhino na kutoka suluhu na Boma fc, huku AFC wakibaki na alama mbili walizopata ugenini dhidi ya Geita Goldmine na Mgambo Shooting

Arusha. Arusha United ‘wana utalii’ imewatambia ndugu zao wa Arusha FC kwa kuwafunga bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

AFC ilitawala muda wote wa mchezo huo, kabla ya Ishara Juma kuwanyamazisha kwa kufunga bao pekee kwa Arusha United katika dakika 90.

Kocha wa Arusha United, Fred Felex Minziro amesema ushindi huo si wa bahati mbaya kwani kampeni yao ya kwenda Ligi Kuu msimu ujao imeanza.

"Wachezaji wangu walikuwa vizuri katika kuhakikisha tunashinda mechi hii, lakini walicheleweshwa kidogo na dakika za mwisho lengo limetimia kwa kufunga bao."

Kocha wa AFC, David Nyambere alisema uamuzi wa waamuzi ndio yamewakwamisha kushinda mechi hiyo, lakini wanamshukuru Mungu wachezaji wako vizuri na wanaahidi kufanya vizuri mechi zijazo.