Arusha FC yetema cheche, yaigeuzia kibao Arusha United

Muktasari:

Timu za Arusha FC na Arusha United zitacheza mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Jumamosi wiki hii.

Arusha. Katibu Mkuu wa Arusha FC Frederick Lymo alisema mchezo utakuwa mgumu, lakini watapambana kupata ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

Arusha. Baada ya kuambulia pointi mbili katika mechi mbili, Arusha FC imepanga kumalizia hasira zake dhidi ya mahasimu wao Arusha United, Jumamosi wiki hii.

Timu hizo zinazotumia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, zitachuana katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza.

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Arusha FC, Frederick Lyimo alisema mechi hiyo ni muhimu kushinda, baada kuvuna pointi mbili badala ya sita ilipovaana na Geita Gold Mine na Mgambo Shooting.

Timu hiyo ilitoka sare ya bao 1-1 Geita Gold Mine kabla ya kupata idadi kama hiyo ilipovaana na Mgambo.

Lyimo alisema pointi mbili dhidi ya Geita Gold Mine na Mgambo, ilizopata ugenini  zitakuwa chichu ya kupata matokeo mazuri dhidi ya Arusha United.

“Jumamosi tutakuwa wageni wa Arusha United tuna imani tutashinda hasa baada ya kupata pointi za ugenini, mkakati wetu ni kufanya vizuri katika mechi zote,” alisema Lyimo.

Hata hivyo, mechi hiyo haitakuwa rahisi Arusha FC kupata ushindi kwa kuwa wapinzani wao watataka pointi tatu, baada ya kuvuna tatu katika mechi mbili zilizopita.

Arusha United iliilaza Rhino Rangers mabao 2-1 kabla ya kutoka suluhu na Boma ya Mbeya katika mechi iliyofuata. Mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza yameendelea kushika kasi kwenye viwanja tofauti nchini.