Arusha United : Tunaisubiri adhabu

Muktasari:

  • Baada ya kutangaza kujitoa, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Steven Mnguto alisema timu hiyo itakabiliwa na adhabu ya kushushwa daraja na kulipa faini kauli ambayo uongozi wa Arusha United wamesema wapo tayari kwa adhabu yoyote itakayotolewa juu yao.

ARUSHA.UONGOZI wa Arusha United ‘Wana Utalii’, umesema uko tayari kupokea na kutumikia adhabu yoyote itakayotolewa na Bodi ya Ligi (TPLB) juu ya uamuzi wao wa kujiondoa kwenye michuano ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Arusha United imejitoa kwa kile walichodai kuwa bodi hiyo imekosa weledi katika uendeshaji wa mashindano hayo hasa kushindwa kuchukua hatua sahihi za matukio ya unyanyasaji, ukatili na hujuma za wazi wazi zinazofanywa na timu wenyeji katika viwanja vya ugenini.

Baada ya kutangaza kujitoa, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Steven Mnguto alisema timu hiyo itakabiliwa na adhabu ya kushushwa daraja na kulipa faini kauli ambayo uongozi wa Arusha United wamesema wapo tayari kwa adhabu yoyote itakayotolewa juu yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Arusha United, Otte Beda Ndaweka aliliambia Mwanaspoti kuwa wamepeleka barua ya kujitoa ofisi za shirikisho hilo na sasa wanasubiri majibu ya adhabu itakayotolewa.