Arteta amfungia vioo staa Ozil

London, England. MAMBO bado magumu kwa kiungo wa Arsenal, Mesut Ozil, ambaye maisha yake yamehamia eneo la wachezaji wa akiba pale Emirates.

Kwa muda mrefu sasa Ozil amekuwa akiwekwa benchi na kocha Mikel Arteta na tangu Ligi Kuu England iliposimama mwezi Machi kupisha corona na baadaye kuanza kwa msimu mpya, Ozil hajaanza hata mechi.

Lakini, katika kuonyesha kuwa hahitajiki, supastaa huyo anayelipwa pesa ndefu kwenye Ligi Kuu England kwa sasa, Pauni 350,000 kwa wiki, hayumo kwenye kikosi cha wachezaji wa Arsenal watakaoshiriki Europa League msimu huu.

Mbali na Ozil, staa mwingine aliyetemwa kwenye kikosi hicho cha Europa League ni Sokratis Papastathopoulos, jambo linaloashiria kuwa atakuwa anasubiri dirisha dogo la usajili ili kwenda kutafuta malisho mapya.

Sokratis, beki wa kimataifa wa Ugiriki, ambaye ilitarajiwa kuachana na miamba hiyo ya Emirates katika dirisha lililofungwa, hakujumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 25 wa Arsenal kwa michuano ya Europa League.

Kwa upande wake, Ozil amekaririwa mara kadhaa akisema kwamba, ataendelea kuwepo Arsenal hadi mkataba wake utakapomalizika. Kwa sasa amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake huku taarifa zingine zikidai kuwa kuna mazungumzo ya kuvunja mkataba yanaendelea.