Arsenal yawapiga pini Aubameyang, Lacazette

Muktasari:

Washambuliaji hao kila mmoja anapokea Pauni 180,000 kwa wiki, lakini sasa Arsenal wanataka kuwapa muda zaidi wa kubaki kwenye klabu yake kwa kufanya marekebisho kwenye mikataba yao.

London, England. Arsenal wamepanga kuwaongezea mikataba mipya mastraika wake pacha Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette, lakini hawatawaongeza mishahara.

Badala yake, wababe hao wa Emirates wamepanga kuwapa bonasi kubwa zaidi kama watafikia viwango walivyojipangia, hasa kwenye kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya mwakani.

Washambuliaji hao kila mmoja anapokea Pauni 180,000 kwa wiki, lakini sasa Arsenal wanataka kuwapa muda zaidi wa kubaki kwenye klabu yake kwa kufanya marekebisho kwenye mikataba yao.

Mkataba wa Aubameyang utafika mwisho 2021, wakati Lacazette atakuwa kwenye kikosi hicho kwa miaka mitatu zaidi kutoka sasa. Pacha hao kwneye fowadi walifunga mabao 50 msimu uliopita.

Bonasi kubwa watakayolipwa ni kama watairudisha timu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo timu itakuwa na uhakika wa kupata makusanyo ya Pauni 40 milioni kila mwaka kwa kufanya hivyo. Lakini, pia bonasi kubwa watalipwa wakati hao kama watashinda ubingwa wa Europa League na Kombe la FA na idadi fulani ya mabao.

Mkurugenzi wa soka kwenye klabu hiyo, Raul Sanllehi na mkurugenzi mkuu Vinai Venkatesham hawataki wachezaji waingia kwenye miezi 18 ya mwisho ya mkataba wao na hivyo kugomea kusaini dili mpya kitendo kinachowafanya kulazimika kuwauza ili wasipate hasara.

Arsenal mpango wao ilikuwa kuwauza Mesut Ozil na Henrikh Mkhitaryan, wanaowalipa Pauni 350,000 na Pauni 160,000 kwa wiki mtawalia, lakini sasa wakali hao wote wataendelea kubaki kwenye timu hiyo huku mikataba yake ikitarajia kufika mwisho 2021.