Arsenal yakomaa na Partey, yamtumia Torreira kumnasa

ARSENAL inataka kumtumia kiungo wake kutoka Uruguay, Lucas Torreira ili kufanikisha mchakato wa kuinasa saini ya kiungo wa Atletico Madrid na timu ya Taifa ya Ghana, Thomas Partey katika dirisha hili.

Arsenal inataka kumtoa Torreira ili kukwepa kutoa kiasi kikubwa cha pesa ambacho kipo kwenye mkataba wa Pertey.

Hii ni mara ya pili kwa miamba hiyo kujaribu kufanya hivyo baada ya mara ya kwanza kumtumia Alexandre Lacazette, lakini Atletico ilikataa na kusisitiza kuwa inahitaji pesa na sio mabadilishano ya wachezaji.

Torreira mwenye umri wa miaka 24, amekuwa hapati nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Arsenal tangu Kocha Mikel Arteta achukue rasmi kibarua cha kuinoa miamba hiyo, hivyo Arsenal imekuwa ikijaribu kumuuza ili kusajili mchezaji mwingine ambaye atakuwa chaguo la kocha.

Usajili wa Partey unaweza kuwa bora zaidi Arsenal kutokana na kiwango chake msimu uliopita.