Arsenal wapo siriazi kwa Gelson

Muktasari:

  • Arsenal imepanga kuingilia kati kumaliza utata unaomhusu winga wa Atletico Madrid, Gelson Martins ili akakipige huko Emirates.

LONDON, ENGLAND. ARSENAL inaonekana kuwa siriazi kwenye mipango yao ya usajili wa mastaa wapya kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa wachezaji mwishoni mwa msimu huu.

Wikiendi iliyopita kocha Unai Emery aliripotiwa kwenda huko Hispania kufuatilia mpango wa kumng'oa staa mmoja kutoka kwenye kikosi cha Valencia. Lakini, wakati hilo likiendelea, kuna staa mwingine huko huko Hispania, Arsenal imeonyesha dhamira ya dhati kabisa ya kupata saini yake.

Arsenal imepanga kuingilia kati kumaliza utata unaomhusu winga wa Atletico Madrid, Gelson Martins ili akakipige huko Emirates.

Winga Gelson kwa sasa anakipiga kwa mkopo huko AS Monaco, lakini uhamisho wake umesababisha malumbano makubwa baina ya Atletico na klabu yake ya zamani ya Sporting CP ya Ureno.

Sporting bado inasubiri kulipwa fidia yao na Atletico baada ya uhamisho wa mchezaji huyo kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.

Lakini, ripoti zinadai Arsenal inataka kumaliza utata kwa maana ya kupeleka ofa ya kuzilipa klabu zote hizo mbili wao wamchukue staa huyo wa kimataifa wa Ureno akakipige kwenye kikosi chao.

Jambo hilo litawaingiza vitani pia na Monaco kwa sababu kocha wao Leonardo Jardim bado anaihitaji huduma ya mchezaji Gelson na huenda akapambana ili abaki kwenye kikosi chake.