NYUMA YA PAZIA : Arsenal wameangukia asubuhi ya Krismasi, pesa mkononi

Muktasari:

Mbele yao kuna Mauricio Pochettino. Mbele yao kuna Max Allegri. Na sasa mbele yao kuna Carlo Ancelotti. Lakini pia kumbuka kwamba Mikel Arteta yupo kazini kama kocha msaidizi pale Manchester City ila anapatikana sokoni.

NAMKUMBUKA Mzee Kumwembe akinipa Sh10 kwa ajili ya kutumia katika sikukuu ya Krismasi takribani miaka 30 iliyopita. Ilikuwa pesa nyingi nyakati hizo. nyakati zimekwenda wapi? Ningeweza kununua vitu vingi vya kula.

Tatizo lilikuwa chaguo. Nile ice cream? Ninywe soda? Ninunue biskuti? Dunia ilikuwa mkononi mwangu. Hauwezi kula kitu. Inabidi uchague kitamu zaidi. Ndivyo ilivyo kwa klabu inayoitwa Arsenal kwa sasa. Wameamkia asubuhi kama hii ya Krismasi. Wana pesa mkononi na wanatafuta bidhaa. Wamemfukuza Unai Emery lakini mbele yao wamekutana na majina kadhaa ya makocha mahiri ambao hawana kazi.

Mbele yao kuna Mauricio Pochettino. Mbele yao kuna Max Allegri. Na sasa mbele yao kuna Carlo Ancelotti. Lakini pia kumbuka kwamba Mikel Arteta yupo kazini kama kocha msaidizi pale Manchester City ila anapatikana sokoni.

Waanze na nani? Pochettino? Inadaiwa kwamba anaweza kukubali kufanya kazi Arsenal licha ya kwamba ametoka kufanya kazi na wapinzani wao wakubwa Tottenham. Tangu afukuzwe hajawahi kusema kwamba hawezi kufanya na Arsenal.

Aliwahi kudai siku nyingi kwamba hawezi kufanya kazi na Arsenal na Barcelona kutokana na kuwa karibu na klabu za Tottenham na Espanyol. Hata hivyo, maisha ya makocha na wachezaji yanabadilika haraka. Jose Mourinho aliwahi kusema hawezi kufanya kazi na Spurs. Leo yuko wapi?

Pochettino anaweza kuwabadili Arsenal. Tatizo kubwa na la msingi ni kwamba hajawahi kutwaa taji lolote maishani mwake. Ana uwezo mkubwa, lakini je ni kocha wa mataji? Mashabiki na mabosi wa Arsenal watakuwa na shaka kuhusu hilo.

Arsenal wakiwa na pesa yao mkononi katika asubuhi hii ya Krismasi wanaweza kumfikiria Allegri. Hata hivyo watajiuliza maswali mengi kidogo kuhusu yeye. Ana mataji matano ya Ligi Kuu ya Italia ‘Serie A’. Amefika fainali za Ulaya. Ana mataji ya Coppa Italia na mengineyo. Arsenal wanaweza kujiuliza Ligi Kuu ya Italia sio imara kama ya England. Nyakati hizi kocha yeyote anaweza kutwaa mataji ya Serie A akiwa na Juve kama ambavyo anaweza kutwaa mataji ya Bundesliga na Bayern Munich. Wapinzani wa huko ni dhaifu.

Allegri anaweza kuwa amefika fainali mbili za Ulaya lakini anaweza kuambiwa kwamba bado Ligi Kuu ya England ni ngumu kuliko kufika fainali mbili za Ulaya. Hata hivyo ni Arsenal wanaweza kumfikiria zaidi na yeye.

Baada ya hapo Arsenal wanaweza kwenda kwa Ancelotti. Huyu ananukia mataji. Ana mataji mawili ya ubingwa wa Ulaya. Ana taji la klabu bingwa ya dunia. Ana taji la Serie A. Sidhani kama Arsenal watakuwa na kikwazo chochote kwake.

Katika soka la Kiingereza, Ancelotti ametwaa Ligi Kuu ya England akiwa na Chelsea. Hauna sababu yoyote ya kuachana na Ancelotti. Unaweza kuwafikiria mara mbili Pochettino na Allgeri lakini sio Ancelotti. Hata hivyo Arsenal wameamkia asubuhi ya Krismasi wakiwa na pesa mkononi. Wana machaguo mengine kando ya Ancelotti na wana muda wa kujiuliza zaidi.

Baada ya hapo unamtazama Arteta. Huyu anaonekana kuwa ‘akili nyingine’ inayotumika zaidi na Pep Guardiola kwa sasa. Mara kadhaa Pep amekaririwa akidai kwamba Arteta ameiva na anaweza kurithi kiti chake kama akiondoka City.

Hapa Arsenal watakuwa wamecheza bahati nasibu. Wanaamini kwamba Arteta anaweza kuwafanyia walau nusu ya kazi ambayo Pep ameifanya City na timu yao itakuwa imara kuliko ilivyo sasa. Inawezekana watakuwa sahihi wakiamini hivi.

Lakini pia inawezekana wasiwe sahihi. Kuwa kocha msaidizi ni jambo moja, kuwa kocha wa kudumu ni jambo jingine. Arteta anaweza kupewa mamlaka kamili na akashindwa kuifanya kazi hiyo. Imewahi kutokea kwa makocha wengi tu. Steve McLaren aliwahi kuwa msaidizi wa Sir Alex Ferguson pale Old Trafford. Alifanya kazi kwa mafanikio. Middlesbrough wakaamua kumchukua awe kocha kamili, akawaangusha. Lakini kuna mambo mengi ya kujiuliza kuhusu Arteta. Anaifundisha City chini ya Pep huku akiwa na wachezaji bora walionunuliwa kwa pesa nyingi. Ataweza kufanya kazi kwa staili hii hii akiwa na wachezaji wa Arsenal? Pale Arsenal kuna Kevin de Bruyne kweli?

Wakati mwingine wachezaji huwabeba makocha licha ya ubora wa makocha. Siamini kama Pep Guardiola na Arteta wanaweza kukifanya hiki wanachokifanya wakiwa na wachezaji wa Brighton. Arteta anaweza kuwa na mawazo sawa lakini ni kweli ataibadili Arsenal kwa kiasi hiki? Na sasa Arsenal wana pesa mkononi. Wana muda wa kuchagua. Hawabanwi na mtu. Hata hivyo wakichagua ovyo wanajua kwamba watakuwa wameangukia katika njia ya Manchester United ambayo tangu kuondoka kwa Sir Alex wamebadilisha makocha wanne. Arsenal wakienda ovyo tu wanaweza kujikuta wakimfukuza pia mbadala wa Unai Emery ndani ya miaka miwili tu ijayo.