Arsenal ni mikwara mwanzo mwisho

Muktasari:

  • Kocha msaidizi wa Man United, Mike Phelan alisema anahisi walihitaji kufungwa na Arsenal kwenye mchezo huo ili kujitambua

London, England. Arsenal inaimba nyimbo zao huko. Inawapiga mikwara Tottenham Hotspur kwamba wanakuja kuwashika.

Mashabiki wa timu hiyo wanatamba Manchester United kazi yao imeshakwisha, sasa bado Spurs. Si unajua kichapo cha mabao 2-0 ilichokitoa kwa Man United kimewarudisha Arsenal kwenye Top Four na sasa imebakiza pointi moja tu kuwakamata Spurs kwenye ile nafasi ya tatu, ndio maana wanawaambia, wamekuja kuwashika.

Kocha Unai Emery anacheka tu, huku akidai aliiaminia Arsenal yake ingefanya mambo muhimu katika mechi yao dhidi ya Man United. Anawasifu wachezaji wake kwa kazi nzuri waliyofanya, tena kwa hisia kubwa.

Emery alisema wachezaji wake walikaba vizuri kabisa kwenye mechi hiyo, huku washambuliaji wakifanya kazi iliyostahili, lakini pongezi zake kubwa zikienda kwa kipa Bernd Leno, aliyekuwa kwenye kiwango bora kabisa, sambamba na mabeki wake Laurent Koscielny na Sokratis, ambao makali yao yameifanya Man United kupoteza mechi yao ya kwanza kwenye ligi tangu Desemba.

“Sasa tunatakiwa kutulia, kuwa watulivu na kuendelea na huu moto,” alisema Emery.

“Tunafahamu, hii mechi ni kama ile tutakayocheza Alhamisi. Mechi moja tu inaweza kubadili kila kitu. Kubaki kwenye kiwango chetu ndio jambo muhimu.”

Straika, Pierre-Emerick Aubameyang, aliyepiga bao la pili kwa mkwaju wa penalti alisema anamshukuru patna wake, Alexandre Lacazette kwa kusababisha penalti hiyo kisha akampa yeye mpira apige. Auba alikosa penalti katika mchezo uliopita kwenye ligi, lakini Lacazette hakuona shida kumwaamini na kumpa nafasi ya kupiga.

“Nilijiamini na wachezaji wenzangu walinifanya nijiamini zaidi. Laca amenipa mpira nipige penalti, hapo nikajiweka sawa zaidi,” alisema Aubameyang.

“Nilifanya makosa dhidi ya Tottenham, nilitazama chini wakati napiga na sikumwaangalia kipa Hugo Lloris, lakini hapo nilimwaangalia kipa hadi mwisho na kufunga penalti yangu.”

Jambo hilo la Lacazette kumpa mpira Aubameyang ili apige penalti limemfurahisha staa wa zamani wa timu hiyo, Ian Wright na kusema wawili hao wameonyesha urafiki mkubwa na namna walivyoshibana uwanjani.

Kocha msaidizi wa Man United, Mike Phelan alisema anahisi walihitaji kufungwa na Arsenal kwenye mchezo huo ili kujitambua, lakini sasa vita inaendelea. Kichapo hicho kimewashusha Man United hadi kwenye nafasi ya tano, lakini watashuka zaidi hadi kwenye namba sita kama Chelsea itashinda mechi yao ya kiporo dhidi ya Brighton.