Arsenal mpo? Majembe ya bure hayo jibebeeni!

Muktasari:

Hata hivyo, hao si mastaa wa nguvu pekee wanaopatikana bure kwenye dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

LONDON,ENGLAND.ARSENAL mpo? Mnataka mpewe nini tena? Dirisha la usajili ndilo hilo limefunguliwa na kuna mastaa kibao wa maana mikataba yao imemalizika na wanapatikana bure kabisa.

Hii inawahusu zaidi Arsenal zaidi baada ya kuripotiwa kwamba bajeti yao ya usajili kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi haizidi Pauni 50 milioni.

Pengine bajeti hiyo ndogo kwa Arsenal imekuja katika kipindi mwafaka kutokana na mastaa wengi wa maana kupatikana bure na Kocha Unai Emery kazi ni kwake tu kujibebea watu wa maana wakakipige Emirates.

Mastaa kama Ander Herrera, Antonio Valencia na Alberto Moreno wanapatikana bure na pengine kwa sasa Vincent Kompany.

Hata hivyo, hao si mastaa wa nguvu pekee wanaopatikana bure kwenye dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

Adrien Rabiot - PSG

Kiungo Adrien Rabiot ni moja ya mastaa wa maana kabisa katika soka la dunia ambaye atapatikana bure kabisa kwenye dirisha hili la usajili baada ya mkataba wake kumalizika huko PSG. Kuna wakati staa huyo alikuwa akihusishwa na Manchester United, Barcelona, Liverpool, Bayern Munich, AC Milan na Juventus, lakini Arsenal wanaweza kuchangamkia fursa ya kumsajili Mfaransa huyo.

Diego Godin- Atletico Madrid

Beki huyo wa kati kisiki ameamua kuachana na maisha ya Atletico Madrid mwishoni mwa msimu huu na kitu kizuri ni kwamba timu yoyote inayomtaka itambeba bure kabisa.

Inter Milan ndio ilikuwa ikimfukuzia kwa karibuni, lakini ukweli upo palepale mwenyewe hawezi kugomea nafasi ya kwenda kucheza kwenye Ligi Kuu England, hivyo Arsenal ikiwa siriazi kumchukua, inamnasa bila shida.

Mario Balotelli- Marseille

Straika Mario Balotelli amekuwa kwenye kiwango bora kabisa huko kwenye Ligue 1, akikipiga kwenye kikosi cha Marseille. Lakini, mkataba wa mchezaji huyo utafika tamati mwishoni mwa msimu huu, hivyo kama Marseille hawatamkabiza kwenye timu yake atakuwa huru kwenda kujiunga na timu nyingine yoyote.

Kwenye timu hiyo amefunga mabao manane katika mechi 12, hivyo Arsenal itapiga bao ikimnasa.

Hatem Ben Arfa - Rennes

Tangu alipojiunga na Rennes mwaka jana, Ben Arfa amekwua kwenye kiwango bora kabisa na hakika ule ufundi wake kwenye kuuchezea mpira upo vilevile.

Staa huyo wa zamani wa Newcastle United hakuwa akipewa nafasi huko PSG na hivyo aliamua kwenda kujiunga na Rennes bure. Miguu ya Ben Arfa bado ina kitu kikubwa inachoweza kukifanya, hivyo Arsenal ataisaidia ikimsajili.

Filipe Luis - Atletico Madrid

Beki wa kushoto Filipe Luis aliamua kurudi Atletico Madrid baada ya kushindwa kufanya vyema huko kwenye kikosi cha Chelsea msimu wa 2014-15.

Badaa ya kutua tu Atletico ubora wake ulirudi kwenye kiwango chake na kuwa mmoja wa wachezaji muhimu kabisa. Lakini mwisho wa msimu huu mkataba wake unakwisha na mchezaji huyo anapatikana bure huku Barcelona na PSG zikipiga hesabu za kumsajili.

Arjen Robben- Bayern Munich

Winga matata kabisa, Arjen Robben maisha yake yamefikia mwisho huko Bayern Munich baada ya kucheza kwa mafanikio makubwa katika kipindi cha misimu 10, akiwa amefunga mabao 143 katika mechi 307. Sawa umri wake umekwenda, lakini Robben bado hajazeeka kihivyo, miguu bado ina vitu muhimu vya kufanya hivyo Arsenal ikifanikiwa kuinasa huduma yake watakuwa amejiweka pazuri.

Franck Ribery- Bayern Munich

Pengine umri wake ni miaka 36 na amekuwa akisumbuliwa sana na majeruhi kwa siku za karibuni, lakini Franck Ribery bado anaweza kwenda kufanya kazi kubwa katika klabu nyingine.

Staa huyo wa Ufaransa bado hajafanya uamuzi wa kuhusu maisha yake baada ya kuondoka Bayern, hivyo pengine huu unaweza kuwa wakati mzuri kwa Arsenal kuchangamka kwenda kumshawishi akatua kwenye timu yao. Safari inahitaji mtu mzima.