Arsenal kimenuka huko

Friday April 26 2019

 

LONDON, ENGLAND.KOCHA wa Arsenal, Unai Emery amewaambia wachezaji wake waendelee kupambana ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Matumaini ya Arsenal kumaliza msimu wa Ligi Kuu England ndani ya Top Four baada ya kukumbana na kipigo kingine usiku wa juzi Jumatano walipochapwa 3-1 na Wolves.

Kichapo hicho kinawabakiza Arsenal kwenye nafasi ya tano, pointi moja nyuma ya Chelsea waliopo kwenye namba nne huku mechi tatu zikiwa zimesalia msimu kufika mwisho. Mabao ya Ruben Neves, Matt Doherty na Diogo Jota uwanjani Molineux ndiyo yaliyofanya ndoto zao kuwa ngumu.

Hata hivyo, Emery bado hajakata tamaa akiamini Top Four inawezekana licha ya kwamba Jumapili ijayo atakuwa na shughuli pevu nyingine ya kwenda kucheza ugenini kwa Leicester City saa chache kabla ya Chelsea hawajakwenda kuwakabili Manchester United uwanjani Old Trafford.

Man United nao wapo kwenye kinyang’anyiro hicho cha kuisaka Top Four, ambapo kama watawashinda Chelsea na kisha Arsenal wakakumbana na kipigo basi watakuwa wamezidiwa kwa tofauti ya mabao tu na The Blues huku mechi zikiwa zimebaki mbili.

"Tumepoteza nafasi iliyokuwa mikononi mwetu, lakini tunaweza kuirudisha nafasi hiyo,” alisema Emery, ambaye kikosi chake cha Arsenal kipo nusu fainali kwenye Europa League.

Advertisement

"Tumepoteza mechi mbili kwa Crystal Palace na Wolves, lakini tuna mechi tatu za kucheza kurudisha nafasi yetu.”

 

Advertisement