Arsenal ikijipindua tu Lacazette anaondoka

Muktasari:

Arsenal kwa sasa inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, pointi saba nyuma ya Top Four na pointi 42 nyuma ya vinara Liverpool.

LONDON, ENGLAND . STRAIKA, Alexandre Lacazette ana makubaliano na klabu ya Arsenal kwamba watamruhusu aondoke kwenye timu hiyo kama watashindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Fowadi huyo Mfaransa amebakiza miaka miwili katika mkataba wake wa sasa huko Arsenal baada ya kujiunga na miamba hiyo kwa ada ya Pauni 52 milioni akitokea Lyon mwaka 2017.

Lakini, The Times linafichua kwamba Lacazette ataruhusiwa kuondoka kama Arsenal itashindwa kufuzu kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu wa 2020-21.

Arsenal kwa sasa inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, pointi saba nyuma ya Top Four na pointi 42 nyuma ya vinara Liverpool.

Lakini, kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta hakijapoteza mchezo wowote yangu mwaka huu wa 2020 uanze, hivyo jambo hilo linawapa matumaini na nguvu ya kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Manchester City amefungiwa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu miwili na kama watafeli kwenye rufaa yao basi jambo hilo litafanya timu itakayomaliza nafasi ya tano kupata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kama chama la Pep Guardiola kumaliza msimu ndani ya Top Four. Lakini, Arsenal wanaweza kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2020-21 kama watabeba ubingwa wa Europa League, ambako wamejiweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua ya 16 bora baada ya kuwachapa Olympiacos 1-0 ugenini.

Mechi 5 zijazo za Arsenal

Leo, Alhamisi vs Olympiacos - nyumbani

Machi 2 vs Portsmouth - ugenini

Machi 7 vs West Ham - nyumbani

Machi 14 vs Brighton - ugenini

Machi 22 vs Southampton - ugenini