Arsenal bado weupe au Emery atapindua meza?

Muktasari:

  • Emery, alipata kuwa juu akijivunia kwenda mechi 22 katika mashindano yote pasipo kupoteza hata mechi moja, lakini baada ya Msimu wa Sikukuu inaonekana ya kale ya Arsenal bado yanaendelea kama ilivyokuwa chini ya Arsene Wenger.

KUTOKA orodha ndefu ya mechi zilizochezwa pasipo kufungwa, kukosa fedha za usajili dirisha dogo hadi kupigwa kwenye Ligi ya Europa, kumeanza kuwasononesha mashabiki wa Arsenal, lakini pengine mabaya zaidi hayapo njiani kwao.

Kichapo cha bao 1-0 dhidi ya BATE Borisov kulionyesha Kocha wa Arsenal, Unai Emery, akiwa katika sikitiko kubwa kuliko siku zote tangu ajiunge na klabu hiyo ya London Kaskazini.

Tayari imetupwa nje ya Kombe la FA, inapambana kuipata nafasi ya nne Ligi Kuu ya England (EPL) ikishika ile ya tano nyuma ya Manchester City, Liverpool, Tottenham Hotspur na Manchester United, hivyo kuna hali ngumu kiasi.

inatakiwa ipambane na miamba hiyo na bado chini yake kuna Chelsea inayojitutumua japokuwa majuzi iliipata dhahama ya kupigwa 6-0, bado kocha kama Maurizio Sarri si wa kupuuzwa kwani anaweza akapindua meza kwa mbinu alizokuwa akitumia Napoli.

Kupoteza mechi ile ya Alhamisi dhidi ya Borisov kulipokewa kwa shida sana na mashabiki wa Arsenal na hata kocha wao, kuanzia uwanjani, hapa London, majumbani na hata kwenye nyumba za kuonyesha mpira.

Emery, alipata kuwa juu akijivunia kwenda mechi 22 katika mashindano yote pasipo kupoteza hata mechi moja, lakini baada ya Msimu wa Sikukuu inaonekana ya kale ya Arsenal bado yanaendelea kama ilivyokuwa chini ya Arsene Wenger.

Kupigwa kwao 5-1 na Liverpool na pia 3-1 na Manchester City ni mambo yanayowahuzunisha Arsenal, lakini pia kuna sintofahamu ya kuachwa benchi kwa mchezaji ghali, Mesut Ozil. Arsenal imekuwa ikilaumiwa kwa kushindwa kumiliki vyema mpira na kujilinda vyema, japokuwa pamekuwapo pia nyakati nzuri tangu kuingia kwa Emery aliyeanza kuwatumia kina Matteo Guendouzi lakini pia akipata mengi mazuri kutoka kwa Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette, japokuwa huyu wa mwisho alipewa kadi nyekundu kwenye mechi ya Borisov baada ya kumpiga mchezaji wa pinzani kiwiko. Yalikuwa maumivu mara mbili japokuwa Emery anasema wana dakika 90 za kupindua matokeo wiki hii, tena kwenye Uwanja wa Emirates, akisema ana imani napo na pia sapoti ya mashabiki wake.

Ana mtindo wake ambao hataki ubadilishwe, akitaka wacheze kutokea nyuma; yaani kipa au beki anawaanzishia wenzake huko nyuma, wapande wakipeana pasi taratibu hadi wakati wa kufunga bao uwadie, na si kubutua na kukimbilia mashuti ya mbali mno.

Ni mtindo mzuri lakini huwa na nyakati za hatari, hasa ikiwa beki ya timu inayocheza hivyo ina upungufu. Kama ilivyo kwa Sarri na Jurgen Klopp, ni ngumu kumbadili Emery katika falsafa yake, ukizingatia mafanikio aliyopata akiwapa ubingwa Paris Saint-Germain kabla ya kuachana nao mwaka jana.

Hata hivyo, ushindi dhidi ya Spurs na Chelsea unampa kichwa, ukionesha akiwa na wachezaji sahihi anaweza kufanya vyema lakini vipigo, kama hicho cha huko Belarus, vinaacha wengi wakikuna vichwa vyao, wakivaa na kuvua miwani. Bado ana nafasi ya kurekebisha mambo.

Emery haoni aibu kufanya maamuzi magumu, licha ya muda mfupi aliokaa Emirates, akidiriki kumweka kando mchezaji anayemlipa Pauni350,000, yaani Ozil, ambaye ilikuwa ngumu kumshawishi, hata hivyo, kukubali kuingia mkataba mpya chini ya Wenger.

Ninaangalia hii na kujiuliza huwa makocha wana nini, ninapofananisha na Jose Mourinho alivyokuwa akifanya akiwa na Paul Pogba. Sijaelewa Emery anafikiria nini kuamua hivyo kipindi hiki akiwa na uhaba wa wachezaji mahiri, tena akiwa na wakati mgumu kwenda mbele na wakikosa ubunifu mbele pia. Kushindwa kwake kuwadhibiti wachezaji wenye majina makubwa na waliokuwa wakijidai mno pale PSG, na hivyo kuhatarisha umoja, upendo na ufanisi kweye Dressing Room, ni moja ya sababu zilizomfanya akandoka hapo na sasa anakabiliwa na majanga labda afanikiwe kumpakia Ozil kwenye meli na kumpeleka klabu ya nje ya England.

Lakini pia hakuogopa kuanza kumweka golikipa mkongwe, Petr Cech pembeni taratibu huku mrithi wake hapo Arsenal – Bernd Leno akipewa nafasi yake. Hata hivyo, amekuwa akiwapanga makipa wake tofauti kuendana na mpango wake wa mechi husika. Lakini kuna hali ya Aaron Ramsey, ambaye Arsenal ilikatisha mazungumzo ya mkataba mpya wakati ni mmoja wa viungo mahiri Ulaya katika eneo lake.

Tayari imempoteza kwa sababu amesaini mkataba wa awali na mabingwa wa Italia, Juventus; lakini bora kwa Arsenal hakubaki England, kwani angewaaibisha kwenye mechi za EPL, Kombe la Ligi na FA na wanasema potelea mbali awararue kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).

Emery hakufanya jitihada zozote kuona Ramsey anabaki, lakini pia kuna ukweli ni ngumu kupata fedha nyingi za mambo tofauti kama usajili na mishahara kwa ‘ubahili’ alio nao mmiliki wa hisa nyingi wa Arsenal, Stan Kroenke anayesema hakuwanunua Arsenal kwa ajili ya ubingwa bali biashara. Wakati Emery anaonyesha hana imani na Ozil, tangu aingie ameshasajili kina Bernd Leno (Pauni19.3m), Sokratis (Pauni17.6m), Stephan Lichtsteiner (bure), Lucas Torreira (Pauni26.4m), Matteo Guendouzi (Pauni7m) na Denis Suarez (kwa mkopo kutoka Barcelona) akiwa ametumia jumla ya Pauni 70.3 milioni tu.

Wakati mwingine Emery anafanya kazi huku akiwa ameweka mkono wake mmoja nyuma; alishangaza majuzi aliposema hawangeweza kusajili wachezaji wa moja kwa moja bali kuchukua kwa mkopo tu.

Rekodi ya Emery inaonesha tangu aingie Arsenal amecheza mechi 38, kushinda 23, sare sita na kufungwa tisa, ushindi ukiwa ni asilimia 60.5. Mabao yaliyofungwa ni 74 na kufunga 47. Wakicheza na klabu kubwa tano za juu amepata ushindi mara mbili, sare mbili na kuchapwa mara nne. Si rekodi mbaya, ukizingatia hana muda mrefu wa kuwabadili wachezaji wake anavyotaka.

Bado Arsenal hawajarudiana na Spurs na Man United, hali inayothibitisha bado kuna kazi ngumu kufika nne bora na kufuzu kwa UCL ambayo washabiki wa Arsenal wanaisikia tu kwa miaka miwili hivi sasa. ikiwa nje ya mashindano ya makombe ya ndani Emery anatakiwa kutumia kila mbinu halali kuhakikisha wanarudi UCL, vinginevyo watu watakwenda na ‘hadithi’ zile zile za Wenger.