Arsenal, Man United kuna moto mkali unaambiwa

Muktasari:

Kocha Ole amekuwa akihusishwa na majina ya mastaa wengine wakiwamo mabeki Harry Maguire, Kalidou Koulibaly na Aaron Wan-Bissaka huku viungo wengine anaowataka ni Dan James, Declan Rice na Gareth Bale.

LONDON, ENGLAND.MAMBO ni mengi muda ni mchache. Manchester United na Arsenal zote zimeshindwa kumaliza ligi ndani ya Top Four na sasa mipango yao ya msimu ujao ni balaa unaambiwa.

Makocha wa vikosi hivyo, Ole Gunnar Solskjaer wa huko Old Trafford na Unai Emery wa Emirates watakuwa bize kufanya mabadiliko kadhaa kwenye vikosi vyao ili kuja na nguvu mpya kwa msimu ujao.

Kwa wiki sasa Man United imeripotiwa kujifungia kwenye mazungumzo ya kumnasa Paul Dybala wa Juventus, huku wakipiga hesabu pia za kumnasa kiungo wa Barcelona, Ivan Rakitic ili kuziba pengo la Ander Herrera.

Kocha Ole amekuwa akihusishwa na majina ya mastaa wengine wakiwamo mabeki Harry Maguire, Kalidou Koulibaly na Aaron Wan-Bissaka huku viungo wengine anaowataka ni Dan James, Declan Rice na Gareth Bale.

Kama nyota hao wote watanaswa, basi Man United ya msimu ujao itakuwa na sura mpya kadhaa kwenye kikosi chake cha kwanza ambapo golini anaweza kuendelea kuwa David De Gea, huku kwenye beki kutakuwa na Luke Shaw kushoto, Wan-Bissaka kulia na mabeki wa kati ni Maguire na Koulibaly. Kwenye viungo watatu kutakuwa na Paul Pogba, Rice na Rakitic na kwenda fowadi kulia atakuwa Dybala, kushoto Bale na katikati atakuwa Marcus Rashford.

Kocha Emery, naye bila shaka atakuwa bize kusaka wachezaji anaotaka kuwaongeza kwenye kikosi chake kinachoripotiwa ni huenda kuna mastaa sita wapya wakatua kwenye kikosi chake kwa kuanzia na Juan Mata na Adrien Rabiot anaoweza kuwanasa bure huku akimsaka pia Youri Tielemans na Ryan Fraser wa Bournemouth.

Mipango ya Emery pia ni kumnasa beki wa kati wa Getafe, Djene Dakonam, huku akiwa kwenye nafasi nzuri pia ya kumsajili staa wa Ajax, Hakim Ziyech.

Kama Emery atafanikiwa kunasa huduma za mastaa hao anaowataka, basi kikosi chake cha msimu ujao kitakuwa kama ifuatavyo, ambapo golini atakuwa Leno huku mabeki wake wakiwa Kolasinac kushoto, Hector Bellerin kulia huku mabeki wa kati ni Sokratis na Dakonam, kwenye kiungo kutakuwa na Tielemans, Rabiot na Torreira huku katika fowadi kulia atakuwa Ziyech, kushoto Mata na katikati Pierre-Emerick Aubameyang.

Kama lisemwalo likitokea, basi Arsenal na Manchester United zitakuwa zimetengeneza vikosi ambavyo bila ya shaka vitachuana vikali na kukamatia ile Top Four baada ya msimu huu uliomalizika hivi karibuni kuambilia patupu zikishika nafasi za tano na sita kwenye msimamo huo wa Ligi Kuu England.