Angola, Cameroon waviziana nusu fainali ya Afcon

Muktasari:

  • Makocha wa timu zote wameonyesha kuhofiana kuelekea katika mchezo huo.

Dar es Salaam. Makocha wa Cameroon na Angola kila moja anahofia mchezo huo wa nusu fainali ya mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17utakaochezwa kesho saa 1:30 usiku kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kocha mkuu wa Cameroon, Libiih Thomas alisema mchezo wao dhidi ya Angola utakuwa mgumu kutokana na wapinzani wao kuwa imara kila idara.

"Angola sio timu nyepesi inapokuwa uwanjani, wapo kamili kila sehemu lakini kwasababu tunacheza nao inabidi tupambane uwanjani kuhakikisha tunapata matokeo," alisema Libiih.

Aliongeza amekuwa akiwaandaa vijana wake kimwili na kiakili ili kuwa bora muda wote katika mechi hiyo.

Naye kocha mkuu wa Angola, Pedro Goncalves wakati wanaanza fainali hizi walikutana na timu nyingi, lakini walipambana vya kutosha kuhakikisha wanafika mbali.

"Cameroon wana miili mikubwa na wanapambana kwa nguvu, tuliwaona walipocheza na Morocco najua kabisa mchezo wetu utakuwa mgumu kwa vijana wangu, lakini tutahakikisha tunapambana," alisema Pedro.