Andrew Vicent 'Dante' aliyeachiwa urithi na Cannavaro jangwani

Muktasari:

  • Nyumbani kwake kumetawaliwa na ukimya kiasi cha kuliaminisha Mwanaspoti ndio maana hata mchezaji mwenyewe hana maneno mengi anapokuwa uwanjani, zaidi ya kupiga kazi kiuhakika.

BEKI Andrew Vincent ‘Dante’ amekuwa mtulivu pindi anapokuwa uwanjani. Yuko vizuri katika kujipanga eneo husika na pia katika ukabaji amekuwa akielewana vizuri na mabeki wenzake wa Yanga, Kelvin Yondani ‘Cotton’ au Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

Lakini utulivu huo haukuishia tu ndani ya uwanja, Mwanaspoti lilimpiga kambi nyumbani kwake Mitaa ya Kijichi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kugundua utulivu wake akiwa nyumbani.

Nyumbani kwake kumetawaliwa na ukimya kiasi cha kuliaminisha Mwanaspoti ndio maana hata mchezaji mwenyewe hana maneno mengi anapokuwa uwanjani, zaidi ya kupiga kazi kiuhakika.

MTAANI SAFI TU

Baada ya Mwanaspoti kufanikiwa kufika mpaka anakokaa Dante, utulivu ulionekena kuwa mkubwa huku kila mmoja akiwa bize na mambo yake. Unaweza kusema mtaa mzima kama masaki fulani hivi.

Baada ya Mwanaspoti kumuuliza kuhusu ukimya huo, Dante alifunguka aliamua kujichimbia huko ili apate muda wa kutuliza akili pindi anapokuwa likizo baada ya kutimiza majukumu yake.

DANTE ATAKA NDOA

Wakati Mwanaspoti likipiga stori mbili tatu na Dante ghafla alitokea mrembo mmoja matata na kusalimia. Ndipo Dante alipotoa utambulisho kuwa huyo ni kichuna chake wa muda mrefu.

Kama desturi za Kiafrika zilivyo, mlimbwende huyo aliandaa chai, muda huo Dante alikuwa ametoka mazoezi, hivyo anahitaji kitu cha kuweka tumboni ili mambo mengine yaendelee.

“Huyu ni mchumba wangu wa muda mrefu anaitwa Sophia Khatib, nipo naye takribani miaka miwili na miezi yake, tumetulia vizuri na tunachokiwaza hivi sasa ni ndoa tu,” alisema.

Kama vile haitoshi, kwa muda ambao wawili hao wamedumu kwenye uhusiano, kitu pekee ambacho wamebakiza ni kutimiza ndoa ili maisha mengine yaendelee.

‘Kweli kitu pekee ambacho kimebaki ni ndoa tu,’ alisema Dante.

Wakati akizungumza hayo mchumba wake aliinuka katika kochi na kutoa vyombo mezani. Mwanaspoti lilibaini sura yake ya upole iliyojaa aibu za kumwaga. Labda ni kutokana na aibu hizo, hakurejea tena kwenye meza ya mazungumzo, aliishia zake jikoni.

RATIBA YAKE USIPIME

Beki Dante aliliambia Mwanaspoti anapokuwa nyumbani huwezi kukaa bila ya kufanya mazoezi. Tena anajipangia ratiba ambayo ataifuata, kwani hawezi kukaa bila kufanya mazoezi kabisa.

“Asubuhi huwa nafanya mazoezi ya kukata tumbo na Push- Up ili kuuweka mwili wangu sawa, baada ya hapo ndio shughuli nyingine zinaendelea hapa nyumbani,” alisema.

Staa huyo, aliongeza, jioni huwa anakwenda kukimbia kwenye fukwe za Kijichi au gym mara kwa mara. Lakini anapokuwa majeruhi kama wakati huu huishia kupiga Push-Up na mazoezi mengine madogo madogo.

“Ninapotulia, basi nakaa tu naangalia movie zangu za kupigana (action) huwa nazipendelea sana au zile za mwendelezo (series).”

SHAVU LA KIMATAIFA

Wachezaji wengi huwa wanapenda kucheza katika klabu za Simba, Yanga na Azam FC ili kujitangaza katika ulimwengu wa soka, ndivyo ilivyo kwa wengi wao ambao husubiria ofa za timu hizo pindi kinapofika kipindi cha usajili.

Dante aliliambia Mwanaspoti tangu amejiunga na Yanga imeweza kumtangaza na kumfanya kuwa mchezaji mkubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

“Nimejifunza kuwa na nidhamu, pia kujua mchezaji anatakiwa kuishi vipi, nazungumzia nidhamu ya ndani ya uwanja na nje ya uwanja, lakini kubwa Yanga imenifanya kuwa mchezaji mkubwa.”

MIKOBA YA CANNAVARO

Wakati alipotua Yanga akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro, alikutana na changamoto ya namba kutoka kwa Nadir Haroub ‘Cannavaro’ pamoja na Yondan baada ya wawili hao kucheza kwa kuzoeana.

Hata hivyo, Dante anafichua Cannavaro alikuwa anamwelekeza kuwa nidhamu ndio mwongozo wake katika maisha ya mpira.

“Alikuwa ananiambia nidhamu ndio kila kitu, alinitaka nizingatie ndani na nje ya uwanja. Nimekuwa nikiufuata wosia wake,” alisema.

Dante aliongeza baada ya kuondoka Cannavaro, anaendelea kujifunza kwa beki Yondan ambaye anacheza naye pacha katika eneo la beki wa katikati.

WAGENI WAMTESA

Dante alisema wachezaji wa kigeni waliotua kipindi cha nyuma, walimfanya aongeze jitihada ya kujituma kadiri alivyoweza, huku akikiri walikuwa wakimpa changamoto ya kutosha.

Dante aliyepewa jina hilo akifananishwa na beki wa kimataifa Brazil, Dante Bonfim Costa Santos anakiri msimu huu haujawa mgumu kwake kwasababu wachezaji wa kigeni hawapo Yanga tofauti na miaka ya nyuma.

“ Ukiangalia timu yetu zamani ilikuwa na wachezaji wengi wa kigeni na changamoto ya namba ilikuwa kubwa, lakini hivi sasa sio wengi.”

MALENGO YAKE

Kila mchezaji ana malengo yake ili kutimiza kile anachokitaka. Kwa upande wa Dante, mipango yake ni kusonga mbele kimataifa.

Anasema hesabu zake hivi sasa ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na mipango, hiyo ameanza kuipigania kwa kuhakikisha anapambana ili timu yake iweze kuingia katika mashindano ya kimataifa.

“Timu ikiingia katika mashindano ya kimataifa nitaonekana na kujitangaza. Itakuwa fursa nzuri kwangu kupata timu nje ya nchi.”