Amunike hataki utani kabisa

Muktasari:

  • Licha ya kwamba Stars imepata ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde, kocha mkuu Emmanuel Amunike bado ataka kuendelea kukisuka kikosi chake

BAADA ya kuwapa furaha mashabiki wa soka Tanzania kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde, Kocha Emmanuel Amunike, amefunguka bado ana kazi kubwa ya kufanya katika mchezo ujao dhidi ya Lesotho kabla ya kumalizana na Uganda mwakani.

Ushindi huo umeifanya Stars kushika nafasi ya pili ikiwa na alama tano katika Kundi L tano pungufu ya ilizonazo Uganda inayoongoza kundi, huku Cape Verde wakishika nafasi ya tatu na pointi nne huku Lesotho wakiburuza mkia wakiwa na pointi mbili tu.

Amunike alisema, licha ya ushindi huo wa juzi, bado ana kazi kubwa ya kufanya kwa kukaa chini na kuangalia sehemu gani ambayo walikuwa wanafanya makosa ili waweze kufuta. “Katika mchezo wa kwanza tulifanya baadhi ya makosa, ila nilikaa chini na kuangalia namna gani tulikosea na katika mchezo huu tumeweza kujirekebisha, lakini nitakaa chini na kuangalia wapi nilikosea na wapi nilipatia ili tuwe bora mchezo ujao.”

Stars itaifuata Lesotho mjini Maseru, mechi ya kuamua hatma yao baada ya sare ya 1-1 awali.