Amunike atema cheche

Muktasari:

Timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ inatarajia kucheza mchezo wa kufuzu fainali za Afrika dhidi ya Cape Verde leo usiku baada ya kuwasili salama nchini humo.

Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amnunike amesem mchezo utakuwa mgumu, lakini ana matumaini ya kufanya vyema endapo wachezaji wake watafuata maelekezo yake.

Praia, Cape Verde. Timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ imewasili salama katika Jiji la Praia, Cape Verde kujiandaa na mchezo wa kufuzu fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon.

Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike, amesema mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwa kuwa wanacheza ugenini, lakini ana matumaini ya kupata matokeo mazuri.

Amunike alisema kuwa endapo wachezaji watafuata vyema mafunzo na maelekezo yake, ana matumaini Taifa Stars itashinda na kujiweka katika nafasi nzuri kwenye mchezo wa marudiano Oktoba 16.

Kocha huyo alisema mkakati wake ni kushinda ili kufufua matumaini ya kucheza kwa mara ya pili fainali hizo ambapo mara ya kwanza ilicheza mwaka 1980 mjini Lagos, Nigeria ikiwa imepita miaka 38.

“Natarajia kushinda mechi ya kesho kama wachezaji watafuata maelekezo yangu, lakini siku zote mechi za ugenini ni ngumu kwa mgeni. Tutapambana kama tulivyofanya kwa Uganda,” alisema Amunike.

Beki wa kimataifa Abdi Banda anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya Boroka ya Afrika Kusini, alisema ana matumaini Taifa Stars itafanya vyema katika mchezo wa kesho.

“Tunamshukuru Mungu tumefika salama na tumekuja kupambana kwa ajili ya mechi ya keshokutwa (kesho),”alisema beki huyo wa zamani wa Simba.

Taifa Stars iliwasili jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Nelson Mandela saa tano asubuhi kwa muda wa Cape Verde sawa na saa nane mchana Tanzania huku msafara huo ‘ukipokewa’ na joto kali la jiji la Praia.

Nahodha wa Taifa Stars anayecheza Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta na  Simon Msuva anayeitumikia Jadida ya Morocco, wamewasili kuungana na wenzao.

Taifa Stars imefikia Hoteli ya Vipprai iliyopo kando mwa Bahari ya Pacific na ilipokewa vyema na wenyeji wakiwemo mashabiki wa Cape Verde.

Taifa Stars ina pointi mbili katika msimamo wa Kundi L, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Lesotho kabla ya kulazimisha suluhu na Uganda ‘The ‘Cranes mjini Kampala.