Amunike aliyeibeba Stars akiota makubwa Misri-2

Muktasari:

  • Anazungumziaje fainali hizo za Afcon? Yeye na timu yake wamejipangaje? Vipi kuhusu tetesi za kutakiwa kutemwa ndani ya Stars? Endelea nayo...!

JANA Jumapili tulianza mfululizo wa makala ya Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Emmanuel Amunike aliyeiwezesha Tanzania kufuzu kwa mara ya kwanza Fainali za Afcon 2019 baada ya kupita miaka 39 tangu Stars iende katika fainali hizo mwaka 1980 zilipofanyika nchini Nigeria.

Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Nigeria aliyewahi kuwika katika klabu kubwa duniani ikiwamo Barcelona ya Hispania alifichua namna alivyopambana akiwatumia nyota wake kukata tiketi hiyo na leo katika muendelezo wa mahojiano yake na Mwanaspoti anafichua mikakati yake.

Anazungumziaje fainali hizo za Afcon? Yeye na timu yake wamejipangaje? Vipi kuhusu tetesi za kutakiwa kutemwa ndani ya Stars? Endelea nayo...!

HATAKI KUTALII MISRI

Tanzania tayari wamekata kiu waliyokuwa nayo ya miaka 39 kutoshiriki Afcon tangu walivyofanya hivyo mwaka 1980, lakini Amunike anataka kuhakikisha kwamba anaenda nchini Misri siyo kama mtalii.

Amunike anasema anahitaji maandalizi makubwa ya kufanya kabla hajaenda nchini Misri kwasababu anatambua ugumu wa fainali hizo zitakazoanza Juni 21.

“Tulihitaji kuingia Afcon na tumefanikiwa. Kinachofuata sasa ni kujiandaa vya kutosha. Tunahitaji mechi za kirafiki ambazo zitawasaidia wachezaji kabla hatujaenda.

“Tunahitaji mechi ngumu dhidi ya timu zilizotuzidi, lakini tunatakiwa tuangalie ratiba kwasababu timu nyingi zinajiandaa na mashindano haya haya kwahiyo ni ngumu pia muda mwingine kupata timu yenye viwango vya juu kucheza nayo.”

Anasema wanatakiwa watengeneze mipango thabiti itakayowawezesha kufanya vyema katika mashindano hayo na siyo kwenda kushiriki tu.

AWAPELEKA WACHEZAJI WA STARS NJE

Mawakala kutoka kona zote za dunia hufurika katika mashindano ya hadhi hii kusaka vipaji na Amunike anaona hiyo ni fursa nzuri kwa wachezaji kujiuza katika klabu kubwa, jambo litakalolisaidia taifa.

“Tukipata wachezaji wengi zaidi ya hawa wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, litakuwa jambo zuri. Itakuwa faida kwetu na kwao katika maendeleo ya mpira wa Tanzania,” anasema.

Anasema kuwapo kwa nyota kadhaa wanaokipiga Ulaya katika kikosi chake kumeleta kitu cha tofauti hivyo anaomba Mungu ajaalie wachezaji wake wote wafanikiwe kupata mikataba Ulaya.

AFUNGUKIA ISHU YA KUFUKUZWA

Amunike wakati akiwa mchezaji alikuwa siyo mtu wa kukaa sehemu moja. Alikuwa ni mtu wa kuzunguka kutoka timu moja kwenda nyingine.

Anasema katika kutembea kwake daima amekuwa akikutana na presha, hivyo presha katika kazi yake ya sasa siyo jambo geni.

“Nimekutana na presha nikiwa mchezaji, sikukata tamaa, nikakutana na presha nikiwa kocha sikukata tamaa. Najua hii ni kwasababu hakuna anayetaka timu yake ipoteze, timu ikipoteza lazima ujikute katika presha kubwa.”

Anaongeza kuwa kitu anachofanya ni kuhakikisha kinainufaisha timu nzima na taifa zima na siyo kumsikiliza mtu ambaye haitakii mema timu.

Akizungumzia ishu ya kuzungumziwa mpango wa kufukuzwa kazi katika kikosi cha Stars kama angeshindwa kufuzu Afcon, alisema jambo hilo halikumfanya ashindwe kufanya kazi yake kwani anaamini katika jambo analofanya.

“Wakati nasaini mkataba nilikuwa najua kabisa kwamba nakuja kufanya kazi. Kazi hii kuna kufukuzwa na kuendelea pia, kwahiyo hata ikitokea kuwa hivyo sitokuwa wa kwanza kwasababu hata kabla sijaja hapa kulikuwa na kocha pia lakini naye aliondoka, kwahiyo kufukuzwa au kuondolewa ni sehemu ya kazi yetu.”

SPIDI YA MAGUFULI KWAKE MZUKA

Amunike anasema tangu ameingia nchini jambo kubwa ambalo amevutiwa nalo ni spidi aliyonayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli.

“Mimi siyo mtu wa kuzunguka sana kwasababu hapa nimekuja kufanya kazi tu, lakini nimevutiwa sana na namna ambavyo Rais anavyofanya kazi yake kiukweli.

“Amekuwa ni mtu wa kupenda kazi na huku akimtanguliza Mungu mbele, naamini Mungu amemkabidhi maono ya kuiongoza Tanzania,” alisema.

Aliongeza kwamba baada ya kwenda Ikulu na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli, Raisi alionyesha kufurahishwa na timu kufuzu kwa katika mashindano hayo.

“Aliniambia tuzidi kupambana na hicho ndicho kitu ambacho tunaendelea kukipigania. Ngoja tuone itakavyokuwa,” anasema.

“Magufuli ameniamini na amenitamkia kwahiyo naamini kabisa kwamba nafanya kazi kwa ufasaha. Najua siyo kila mtu anaweza kukuamini hata kama ukipoteza au ukishinda.”

APIGA HESABU NDEFU AFCON

Mashindano ya Afcon yanashirikisha timu ambazo zina uzoefu mkubwa, hali hiyo imemfanya Amunike aanze kufikiria mipango mikubwa ambayo itaisaidia timu yake.

“Tunaenda kukutana na timu zenye uzoefu wa mashindano haya kwahiyo sio kitu chepesi. Sawa tumepata tulichokuwa tunakihitaji lakini hivi sasa tunapaswa kujua vile ambavyo tunaenda kupambana.

“Kujituma kwa wachezaji uwanjani ndiyo kitu ambacho Watanzania wanahitaji kuona, kwasababu kila timu iliyofanikiwa ni matunda ya kuvuja jasho.”

Anasema anaamini wachezaji wake watafanya kila linalowezekana kuhakikisha timu yao inafanya vizuri kuendana na uzito wa mashindano hayo.

“Hii ni fursa kwa wachezaji kucheza na kuonyesha kitu gani ambacho wanacho, kuna mawakala wengi watakuwapo kwahiyo ni muda wao kupambana na kujitangaza. Ni fursa kubwa kwao.”

Je unajua safari ya Amunike katika soka ilianzaje na alitumia mbinu gani kusajiliwa Barcelona ile ya Pep Guardiola na Luis Enrique? Usikose nakala yako ya Mwanaspoti kesho.