Amri Said hana presha Mbeya City

Dar es Salaam. Licha ya mashabiki wa Mbeya City kuzidi kupiga kelele kutaka kocha Amri Said ‘Stam’ ang’oke ndani ya kikosi hicho kutokana na matokeo mabaya, lakini mwenyewe amesema hana presha kama uongozi utaridhia hilo ataachia ngazi.

Mbeya City inashika mkia kwenye msimamo wa ligi ikiwa ndiyo timu pekee ambayo haijashinda mchezo wowote kwenye Ligi Kuu Bara wala kufunga bao lolote.

Katika michezo mitano iliyocheza mpaka sasa imeambulia pointi moja tu ilipotoka suluhu na watani zao wa jadi Prisons hivyo mashabiki klabu hiyo kwenye mitandao ya kijamii na hata wakiwa viwanjani kwenye michezo inayohusu kikosi hicho wakitaka kocha huyo atimuliwe.

Pia kutimuliwa kwa kocha wa Ihefu,Maka Mwalwisi hivi karibuni,ndiyo kunachochea mashabiki wa Mbeya City kuutaka uongozi wa timu hiyo nao kufanya maamuzi magumu dhidi ya Amri.

Hata hivyo, Amri amewataka mashabiki hao kuwa wavumilivu kwani anaamini kikosi hicho muda si mrefu kitakuwa katika kiwango bora.

“Nasikia maneno mengi dhidi yangu, lakini ninachoomba ni kwamba mashabiki wawe wavumilivu kwani tunaijenga timu, wachezaji wengi ni wapya,” alisema Amri.