Amri Said atimuliwa Mbeya City

Muktasari:

Mbeya City inashika nafasi ya mwisho katika msimamo wa Ligi ikiwa na pointi mbili tu.

KOCHA Amri Said amefungashiwa virago usiku wa leo katika klabu ya Mbeya City baada ya kupata matokeo mabaya mfululizo tangu mwanzoni mwa msimu huu.

Kupitia mtandao wa Instagram wa ukurasa rasmi wa Mbeya City, umeweka taarifa hiyo ukiwajulisha mashabiki wake kwamba imeachana na timu yake huku leo mchana wakitoka kupokea kichapo cha 2-1 dhidi ya Mwadui Fc, mchezo uliopigwa katika uwanja wa Mwadui Complex.

"Maamuzi haya yamefanyika baina ya pande mbili baada ya majadiliano kutokana na muenendo wa kutoridhishwa na muenendo wa timu yetu inayoshiriki Ligi Kuu," ilieleza taarifa hiyo ambayo ilionyesha kutolewa na Afisa mtendaji mkuu, Emmanuel Kimbe.

Kuondoka kwa Amri Said, taarifa hiyo ilieleza kwamba nafasi yake itashikiliwa na kocha msaidizi, Mathias Wandiba.

Amri alijiiunga na Mbeya City msimu uliopita katika mzunguko wa pili na alihakikisha timu hiyo inasalia katika Ligi Kuu.

Licha ya kuweza kuipambania katika msimu uliopita, msimu huu umekuwa mbaya kwake baada ya kushika nafasi ya mwisho huku wakiambulia pointi mbili tu.