Breaking News
 

Amir Khan auchokoza muziki Manny Pacquiao

Monday September 10 2018

 

London England. Bondia mahiri wa Uingereza anayeishi Marekani, Amir Khan ameomba pambano dhidi ya mbabe wa uzani wa Welter, Manny Pacquiao.

Khan ametaka pambano dhidi ya Pacquiao baada ya kumshinda kwa pointi Samuel Vargas walipozipiga wikiendi iliyopita kwenye ukumbi wa uwanja wa Arena Birmingham.

Licha ya ushindi lakini bondia huyo mwenye miaka 31, hajaonyesha kiwango bora kwani alianza kupelekwa sakafuni katika sekunde ya pili ya raundi ya pili.

Khan alishinda kwa majaji wote watatu waliompa pointi 119-108, 119-109 na 118-110, muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi na kushuka ulingoni alipaza sauti akisema anamtaka Pacquiao.

“Ninataka kupigana na Manny ‘Pacquiao’ huyu ndiye bondia wa hadhi yangu,” alisema Khan.

Wengi wa wadau wanaamini kuwa Khan anamtaka Pacquiao kwa sababu ya kutaka kujitengenezea fedha lakini hana uwezo wa kumkabili mbunge huyo wa Ufilipino mwenye ngumi nzito na kasi muda wote wa pambano.

Hilo lilikuwa pambano la pili kwa Khan tangu aliporeja kwenye ngumi baada ya kusimama kwa karibu miaka miwili, alianza kwa kumshinda Phil Lo Greco, Aprili mwaka huu.

Advertisement