Ambundo, Bigirimana noma

Muktasari:

  • Wachezaji hao wamekuwa katika kiwango cha juu tangu walipojiunga na KMC na kuisaidia timu hiyo kupanda hadi nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Bara

KASI ya nyota wa Alliance FC, Dickson Ambundo na Blaise Bigirimana katika Ligi Kuu Bara kwa mujibu wa Kocha Mkuu wao, Malale Hamsini bado kabisa na jamaa hao watashangaza wengi.

Nyota hao pamoja na Hussein Javu wametengeneza safu kali ya timu hiyo ngeni katika ligi hiyo na Kocha Malale alisema huo ni mwanzo tu kwani makubwa kutoka kwao yanakuja.

Akizungumza na Mwanaspoti, alisema alipofika katika klabu hiyo alivutiwa na uwezo wa Ambundo na ndipo akaamua kumtafutia wachezaji ambao wataweza kushirikiana nao ili kuisaidia timu.

“Ambundo ni mchezaji anayejua kufunga na ana spidi anapokuwa uwanjani, ni wachezaji wachache wa aina yake niliokutana nao, ndio maana Javu na Blaise nao wanafanya vizuri,” alisema.

Aliongeza aliamua kumbadilisha nafasi, Bigirimana kutoka nafasi ya winga aliyokuwa akicheza akiwa Stand United na kumfanya ushambuliaji ili aweze kufunga zaidi.

“Nataka Ambundo, Javu na Blaise wote wawe wanafunga kila wanapofika langoni, ndio maana hata Blaise alipokuwa anacheza alikuwa anatokea pembeni lakini hapa nimemtengeneza na kumchezesha karibu na bao na anafunga sawa na Ambundo.”

Ambundo ameifungia timu hiyo mabao manne huku Blaise tangu asajiliwe dirisha dogo tayari ameshafunga mawili katika mchezo dhidi ya African Lyon na Ruvu Shooting na kumfanya kurudi kwenye kasi yake ya zamani.