Alliance yaanza kujifua kujiandaa na VPL

Muktasari:

  • Alliance ni miongoni mwa timu nne zinazochuana vikali katika vita ya kukwepa kushuka Daraja, ikiwa inashika nafasi ya 18 katika msimamo wa Ligi Kuu.

Kikosi cha Alliance FC leo Alhamisi kimeendelea na mazoezi yake katika dimba la Nyamagana jijini hapa kwa ajili ya Ligi Kuu inayotarajia kuendelea hivi karibuni.
Timu hiyo ambayo ni msimu wake wa pili kushiriki Ligi Kuu, haipo mazingira mazuri katika msimamo, ambapo katika michezo 29 ilizocheza imekusanya alama 29 na kukaa nafasi ya 18 na kuifanya kuwa kwenye presha ya kujinasua kutoshuka Daraja.
Leo Mwanaspoti Online imeshuhudia kikosi hicho chini ya Kocha Msaidizi, Dady Gilbert kikijinoa katika uwanja huo ikiwa ni siku ya tatu mfululizo tangu Serikali iliporuhusu shughuli za michezo kuendelea.
Licha ya Kocha huyo kutokuwa tayari kuelezea chochote kuhusu mazoezi hayo ,  Mwanaspoti imeshuhudia wachezaji wakifanya mazoezi tofauti, ikiwa ni kupiga mashuti langoni, kukabana na kunyoosha misuli.
Hata hivyo taarifa za kiafya kwa wachezaji, Daktari wa timu hiyo, Abel Shindika hakuweka wazi, huku akieleza kwa ufupi kuwa bado hajakamilisha vipimo kwa kikosi chake na kwamba anaamini kesho atakuwa na majibu.
“Kwa leo niache, bado sijakamilisha vipimo kwa wote, lakini naamini kufikia kesho nitakuwa nimemaliza hili zoezi na kuelezea zaidi” amesema Shindika.