Alliance wawavutia kasi vibonde Ligi Kuu

Muktasari:

Singida United wanashika mkia kwenye msimamo wa ligi wakiwa wamekusanya pointi 11 huku wakichza michezo 23 wakati Alliance wanashika nafasi ya 13 wakikusanya pointi 28.

WAKATI Alliance FC  kesho Jumapili wakiwakabili vibonde wa Ligi Kuu Bara, Singida United, kocha msaidizi wa timu hiyo Mathias Wandiba amesema wataingia kwa tahadhari kuwakabili na kamwe hawatowadharau.
Mpambano huo unatarajiwa kupigwa Uwanja wa Nyamagana jijini hapa ambapo Alliance wataingia wakiwa na kumbukumbu ya kuwachapa Mwadui mabao 4-1kwenye mtanange uliopita.
Singida United wanashika mkia kwenye msimamo wa ligi wakiwa wamekusanya pointi 11 huku wakichza michezo 23 wakati Alliance wanashika nafasi ya 13 wakikusanya pointi 28.

Wandiba alisema wamezungumza na wachezaji wao na kuwaasa kutowadharau wapinzani wao kutokana na matokeo yao kwani soka lolote linaweza kutokea hivyo ni kuongeza umakini.

"Mchezo wa soka unahitaji heshima, kamwe hatutowadharau Singida United kwa sababu ya matokeo yao mabaya, tutaingia kwa tahadhari kubwa ili kupata pointi tatu," alisema Wandiba.

Wandiba alisema kikosi chao kimeanza kuimarika hasa safu ya ushambuliaji jambo ambalo linawapa nguvu ya kuendelea kupambana kwenye ligi.