Alliance waichimba mkwara Yanga Princess

Muktasari:

 

  • Alliance inacheza mechi yake ya tatu mfululizo ikiwa ugenini ambapo imepoteza mchezo mmoja,sare moja na kesho Alhamisi inajitupa tena uwanjani kujiuliza mbele ya Yanga Princess.

Mwanza.ALLIANCE Queens imecheza mechi mbili mfululizo bila kuonja ushindi wowote katika Ligi Kuu ya Wanawake na leo Alhamisi inajitupa uwanjani kuwakabili Yanga Princess ambapo Kocha wa kikosi hicho Ezekiel Chobanka ameapa kuwa pointi tatu ni muhimu.

Timu hiyo ambayo imevuna pointi nne hadi sasa ipo nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi hiyo ambayo kinara wake ni JKT Queens mwenye alama tisa na mabao 31 baada ya mechi tatu.

Mchezo kwa timu hizo unatarajia kuwa mkali kutokana na pande zote kuhitaji ushindi ili kujiweka nafasi ambapo Yanga Princess katika mechi tatu walizocheza wamekusanya alama sita na kukaa nafasi ya sita.

Kocha Chobanka alisema kuwa licha ya kucheza mechi tatu ugenini lakini leo hakuna mzaha wowote na anachohitaji ni ushindi ili kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi hiyo.

Alisema kuwa vijana wake atahakikisha anawaandaa kisaikolojia na fiziki ili watakaposhuka dimbani kuwakabili wapinzani wao wawe fiti na waweze kuondoka na alama tatu muhimu.

“Tumekosa pointi tatu katika mechi mbili zilizopita lakini kesho (leo) lazima tupambane ili kuweza kushinda bado hatuko nafasi nzuri kwahiyo mchezo huo ni muhimu sana”alisema Chobanka.

Kocha huyo aliongeza kuwa kikosi chake hakina majeruhi yeyote ambaye anaweza kuukosa mchezo huo hivyo wapinzani wao wasitarajie mteremko licha ya kupata matokeo mazuri katika mechi iliyopita.

Alisema kuwa malengo yao hayakutimia kwani walihitaji kushinda mechi zote za ugenini lakini hadi sasa wameambulia pointi moja na kwamba bado hawajakata tamaa.

“Tunajua wapinzani wamejiandaa vizuri kwa sababu wameshinda mechi mbili mfululizo tofauti na sisi,kwahiyo tutahakikisha hatufanyi uzembe wowote ili kufikia malengo yetu”alisema Kocha huyo.