Alliance imepania kurejea Ligi Kuu kwa kishindo

MSIMU uliopita Alliance FC ilishuka daraja baada ya kudumu kwa misimu miwili tu Ligi Kuu, ambapo wanajipanga tena kushiriki Daraja la Kwanza ili kukata tiketi ya kurudi kuungana na miamba ya soka nchini, Simba na Yanga.

Alliance ambayo ilikuwa timu yenye ushindani hasa kipindi ikishiriki ligi ngazi za chini ikiwa ngazi ya Mkoa wa Mwanza, Daraja la Pili na la Kwanza kabla ya hali kubadilika ilipopanda Ligi Kuu.

Kwa sasa timu hiyo inajiandaa upya kwa ajili ya kushiriki Daraja la Kwanza, ambapo itashuhudiwa ikiingia dimbani na mabadiliko makubwa hasa ndani ya uwanja.

Timu hiyo msimu ujao imepangwa kundi B ikiwa ni pamoja na Pamba, Mbao (Mwanza), Singida United (Singida), Geita Gold (Geita), Arusha FC (Arusha), Rhino Rangers na Kitayosce (Tabora), Fountain Gate (Dodoma) na Transit Camp ya jijini Dar es Salaam.

Pamoja na ushindani utakaojitokeza katika ligi hiyo, lakini timu hiyo imetamba kufanya kweli ili kurejea tena Ligi Kuu kutokana na maandalizi waliyofanya ikiwamo usajili na mabadiliko.

MAANDALIZI YAO

Baada ya kazi ya usajili wa wachezaji kufungwa, Alliance FC chini ya kocha wake mpya raia wa Kenya, Daniel Solonka ilianza mazoezi ya pamoja, huku ikicheza mechi kadhaa za kujipima nguvu.

Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Stephano Nyaitati anasema uongozi umeweka mipango mizuri ili kuhakikisha kwamba wanatoa sapoti kubwa kwa timu kufikia malengo.

Nyaitati anasema pamoja na kushuka daraja msimu uliopita, lakini maandalizi waliyonayo timu hiyo itarudi haraka Ligi Kuu kwani wamefanya kulingana na mahitaji ya timu.

“Maandalizi kwa ujumla kwa upande wa uongozi tumejipanga vizuri kuhakikisha tunatoa sapoti kwa timu ili kurudi tena Ligi Kuu, tunafahamu ushindani ndio maana tumeweka mipango sawa,” anasema Nyaitati.

Anasema makosa waliyoyafanya msimu uliopita na kusababisha matokeo mabovu waliyopata hawatarajii yajirudie na badala yake watasahihisha ili kufikia malengo yao.

Hata hivyo, kigogo huyo anasema kuna ushindani mkubwa uliopo kwenye Ligi Daraja la Kwanza, huku akisisitiza kuwa wanahitaji kila mechi wapate alama tatu na kutangaza kupanda daraja kabla ligi haijaisha.

“Makosa yaliyofanyika msimu uliopita hadi tunashuka daraja hatutaki yajitokeze tena, tumejipanga kimkakati na tunachotaka ni kuona tunarudi haraka Ligi Kuu.”

USAJILI WAO SASA

Kikosi cha Alliance kinaundwa na wachezaji 30 ambao wamesajiliwa kwa ajili ya msimu ujao unaotarajia kuanza Oktoba keshokutwa kusaka upya tiketi ya kurudi Ligi Kuu. Wachezaji hao walipatikana kupitia mchujo maalumu uliokutanisha nyota wengi kutoka maeneo tofauti na wengine kupandishwa kutoka kikosi B.

Kocha Solonka anasema kutokana na usajili alioufanya wa nyota chipukizi, kuna jambo kubwa watafanya.

“Nimesajili wachezaji 30 ambapo baadhi tuliwapata kwenye mdahalo maalumu na wengine kuwapandisha kutoka timu B, nimeridhika nao kutokana na uwezo wao,” anasema Solonka.

Anasema soka la Tanzania halitofautiani sana na Kenya japokuwa hapa nchini kuna mwitikio mzuri zaidi wa mashabiki kujitokeza viwanjani na kuzipenda timu zao.

“Soka la Tanzania lipo juu kidogo kutokana na amshaamsha ya mashabiki kuzipenda timu zao, mengine ni ya kawaida kwa sababu nina uzoefu wa ligi za ushindani.”