Alliance FC gari limewaka Kirumba!

Muktasari:

Mchezo kwa Kocha wa Alliance leo ni wa tatu,ambapo amefanikiwa kushinda miwili na sare mechi moja.

Mwanza/Musoma. Kocha wa Alliance FC, Dady Gilbert ameendelea kuwapa raha mashabiki wa timu hiyo baada ya leo kuutumia vyema uwanja wao wa nyumbani kwa kuibamiza Mtibwa Sugar bao 1-0.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu raundi ya 14 kila timu ilipambana kwa uwezo wake, lakini Alliance iliweza kuwazidi wapinzani wao na isingekuwa  umakini mdogo katika umaliziaji wa mipira ya mwisho wangeweza kushinda hata zaidi ya bao hilo.
Kipindi cha pili licha ya kosa kosa za hapa na pale,Alliance iliweza kufanya mashambulizi mfululizo na kufanikiwa kupata bao dakika 54 kupitia kwa Dickson Ambundo aliyemalizia krosi fupi ya Michael Chinedu baada ya Kipa wa Mtibwa, Shaban Kado kutema shuti kali ya Siraji Juma.
Kwa matokeo hayo,Alliance wanafikisha pointi 13 na kupanda hadi nafasi ya 15,huku Mtibwa Sugar wakibaki na alama zao 23 katika nafasi ya nne.
Wakati huohuo,mkoani Mara mzimu wa sare umeendelea kuiandama Biashara United baada ya leo kulazimishana suluhu ya bila kufungana dhidi ya Prison ikiwa ni mchezo wa saba bila kupata ushindi,huku ikipoteza mchezo mmoja kwenye uwanja wao wa Karume Musoma.