Alliance, Ndanda kazi imeanza

LIGI Daraja Kwanza (FDL) inaanza leo Ijumaa kwa michezo miwili kupigwa katika harakati za kusaka nafasi ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, African Lyon itaikaribisha Ndanda FC iliyoshuka daraja msimu uliopita na sasa inatupa karata yake ya kwanza kwenye Kundi A.

Mchezo mwingine utakuwa wa Kundi B wakati wageni wa FDL, Fountain Gate ikiikaribisha Alliance iliyoshuka daraja katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Shughuli kubwa ya michezo hiyo ni kuziona timu zilizoshuka daraja kutaka kurudisha heshima yao kwa kupata ushindi kwenye michezo ya leo.

Kocha wa Alliance FC, Daddy Gilbert alisema; “Hatuna hofu maana tumejiandaa vizuri, tunacheza na kuwapa heshima wapinzani wetu kwa kuwa kila timu ina mipango yake, tunachoweza kusema watu wa Dodoma watarajie kupata burudani.”

“FDL ni ligi ngumu na muhimu kwa upande wa maendeleo ya soka maana huku ndiko wanakotoka wachezaji wa timu ya taifa, na hii ni moja ya ligi ambayo mchezaji anayeonyesha uwezo anaweza kutoka kwa kupata timu ya Ligi Ku,” alisema Gilbert.

Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Muya alisema wamekamilisha maandalizi yao na timu iko vizuri kwa kuwakabili wapinzani na ana matumaini watavuna alama katika mchezo wa leo.

“Huu ni msimu wetu wa kwanza kwenye ligi, lakini ndani tuna wachezaji wenye uzoefu ambao watasaidiana na vijana wetu na kuifanya timu kuwa bora zaidi,” alisema Muya.

Ligi hiyo itaendelea kesho kwa michezo miwili ya Kundi A, Njombe Mji ikiikaribisha Mbeya Kwanza kwenye Uwanja wa Sabasaba, na African Sports ikicheza na Majimaji Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Mbeya Kwanza tayari imefanya mabadiliko ya benchi lake la ufundi na sasa inaongozwa na Stephen Mtata ambaye anarekodi tamu ya kufundisha timu kadhaa za FDL huku Michael Mnyali akiwa kocha msaidizi.

Kwenye Kundi B, Kitayosce inayonolewa na Idd Cheche ikiikaribisha Transit Camp Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi na Geita Gold ikicheza na Singida United.

Kocha wa Transit Camp, Emmanuel Gift amejigamba kuwa na timu imara ambayo msimu ujao itakuwa moja ya timu itakayopanda Ligi Kuu.