Alliance, Mbao msikilizeni Chidiebere

Muktasari:

Mbao na Alliance zitaungana na Pamba kucheza Daraja la Kwanza baada ya kushuka daraja ambapo sasa mkoa wa Mwanza utakuwa na timu moja ya Gwambina kwenye Ligi Kuu msimu ujao.

STRAIKA wa Mbeya City, Abasirim Chidiebere amesema Mbao na Alliance wanatakiwa kukomaa vilivyo kama wanataka kufanya vizuri Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao.

Mbao na Alliance zitaungana na Pamba kucheza mashindano hayo baada ya kushuka daraja ambapo sasa mkoa wa Mwanza utakuwa na timu moja ya Gwambina itakayoshiriki Ligi Kuu msimu ujao.

Akizungumza na Mwanaspoti Online, leo Jumatano Agosti 12, 2020, Chidiebere ambaye kwa sasa ameweka makazi yake ya kudumu jijini Mwanza amesema timu hizo zinatakiwa kukomaa ili kurudi Ligi Kuu.

“Nimecheza FDL nikiwa Stand United najua ugumu wake kinachotakiwa Mbao, Alliance na Pamba wakomae ili kufanya vizuri na kupanda Ligi Kuu,”

“Sio jambo nzuri kuona Mwanza inakuwa na timu moja pekee Ligi Kuu hivyo sasa hakuna kulaumiana kilichobaki ni wadau wa soka kuungana na kuzipa sapoti hizi timu ili kupanda daraja.

“Kinachotakiwa ni kuhakikisha hizi timu zinafanya usajili wa nguvu kipindi hiki kwani wanatakiwa kuwa na wachezaji wa kazi maana haya mashindano yanataka nyota wazoefu maana ni magumu sana na yanahitaji uvumilivu,”amesema Chidiebere.

Mshambuliaji huyo raia wa Nigeria amesema kwa sasa ana mkataba na Mbeya City ambao utamfanya awepo hadi msimu ujao wa Ligi Kuu.

“Nina mkataba hapa ila unaniruhusu kuondoka iwapo nikipata timu nyingine kikubwa nimefurahi kuona nimeibakisha hii timu Ligi Kuu niliingia dirisha dogo la usajili lakini nashukuru Mungu nilicheza mechi 14,” amesema Straika huyo.